Breaking News

WAMACHINGA MWENGE WASISITIZA AMANI NA MSHIKAMANO BAADA YA HOTUBA YA RAIS SAMIA KUHUSU RIPOTI YA JAJI CHANDE

Wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga wa eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, wameeleza kufurahishwa na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa mara baada ya kupokea ripoti ya Tume iliyoongozwa na Jaji Othman Chande.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, wamachinga hao wamesema hotuba ya Rais imebeba ujumbe wa matumaini kwa wananchi, hususan vijana, kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini.

Wamesisitiza kuwa hotuba hiyo imewapa matumaini mapya kuhusu mustakabali wa taifa, hasa katika nyanja za amani, ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya kitaifa, pamoja na kuimarika kwa haki na maridhiano.

Mmoja wa wafanyabiashara hao alinukuliwa akisema kuwa hotuba hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi muhimu ya taifa.

Aidha, wamachinga hao wameeleza matarajio yao kuwa mapendekezo yatakayotokana na ripoti hiyo yatachangia kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, sambamba na kuboresha mazingira ya kijamii na kiuchumi.

Kwa ujumla, wamempongeza Rais na serikali kwa juhudi zinazoendelea za kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wa ngazi zote.