EACOP KUENDELEA KUUNGA MKONO MAENDELEO SEKTA YA ELIMU NCHINI
Mratibu wa Mahusiano ya Jamii kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) Bw. Theophil Celestine akitoa cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha Sita katika Shule ya Selondari ya Bunazi iliyopo mkoani Kagera hivi karibuni.
Mratibu wa Mahusiano ya Jamii kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) Bw. Theophil Celestine (wa tatu kutoka kushoto pichani) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa shule ya Sekondari ya Bunazi, walimu pamoja na wanafunzi wa Kidato cha 6 wakati wa mahafali ya Kidato cha 6 shuleni hapo.
Na Mwandishi Wetu, Misenye - Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)imerejea dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono maendeleo sekta ya elimu hapa nchini kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), sambamba na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo namba nne linalohusu elimu bora.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP kwenye mahafali ya Kidato cha Sita katika Sekondari ya Bunazi iliyopo Wilaya ya Misenyi,mkoani Kagera , Bw. Theophil Celestine, ambaye ni Mratibu wa Mahusiano ya Jamii wa EACOP Tanzania, alisema mradi huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
“Mradi wa EACOP mbali ya kujihusisha na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha mafuta ghafi, tunajihusisha pia kuchangia maendeleo ya jamii zinazopitiwa na mradi,” alisema.
“Tunajihisi kuwa na wajibu wa kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya mradi wetu kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na kutekeleza kikamilifu sera ya kutoa kipaumbele kwa wazawa (local content),” aliongeza.
Kama sehemu ya mchango huo, EACOP imeahidi kutoa mashine ya kunakili (photocopy machine) ili kusaidia shughuli za kitaaluma na kiutawala shuleni hapo.
Mbali na kuwasaidia watu waliopitiwa na mradi (PAPs) katika sekta mbalimbali, ikiwemo utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi bila malipo kupitia vyuo vya ufundi stadi na kazi (VETA), EACOP inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kusaidia elimu nchini.
Miongoni mwa programu hizo ni mradi unaojulikana kama (Keep a Girl in School Initiative – Phase I- Kumsaidia mtoto wa kike kuendeleaa kubaki shuleni) chini ya Mpango wa Uwekezaji wa Kijamii na Kiuchumi (SEI), unaolenga kuboresha afya na usafi wa hedhi (MHM) kwa wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari zilizopo kandokando ya mradi wa EACOP nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Arieth Philemon Munisi, aliishukuru EACOP kwa msaada huo, akieleza kuwa unachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Hata hivyo, alibainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, ikiwemo ukosefu wa uzio wa shule, hali inayowaweka wanafunzi—hasa wasichana—katika hatari ya usalama, uharibifu wa mali, na uvamizi usioidhinishwa.
Changamoto nyingine alisema ni ukosefu wa jengo la chakula (dining hall), hali inayoathiri ustawi wa wanafunzi na kupunguza nafasi za mijadala ya kitaaluma pamoja na shughuli mbalimbali za shule.
Aidha, alieleza kuwa jiko la shule lipo katika hali mbaya, jambo linaloathiri maandalizi ya chakula kwa wanafunzi shuleni hapo.
Vilevile, uchakavu wa vifaa vya uchapishaji wa mitihani kama vile mashine za kunakili ( Photocopy machine) na printa umeathiri kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa shughuli za kitaaluma na kuongeza gharama za uendeshaji.
Pia alibainisha kuwa uhaba wa vifaa vya michezo kama jezi, mipira na nyavu unawanyima wanafunzi fursa muhimu za kushiriki katika michezo na shughuli za ziada, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa kujihusisha na mienendo hatarishi.
Aliwataka wadau wengine na wahisani kujitokeza kusaidia kutatua changamoto hizo.
Mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya shule yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wazazi, walezi, walimu na wanafunzi.
Shule ya Bunazi Secondary School ilianzishwa mwaka 1998 na Misenyi Development Association (MIDEA), shirika lililoanzishwa na wakulima wa kahawa kwa lengo la kuimarisha elimu katika eneo hilo. Mwaka 2022, shule hiyo iliingizwa rasmi katika mfumo wa shule za Serikali.
Kwa sasa, shule ina jumla ya wanafunzi 1,332, ambapo 821 ni wasichana na 511 ni wavulana, kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Sita. Shule inapokea wanafunzi wa O-Level kutoka vijiji vilivyo karibu na mradi kama Bulfani, Nyabihanga na Kabwoba, huku wanafunzi wa A-Level wakitoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Mwaka huu, jumla ya wasichana 104 kati ya 110 wamehitimu, huku sita wakihamishwa kwenda shule nyingine kwa sababu mbalimbali.
Shule hiyo ina jumla ya watumishi 51, wakiwemo walimu 42—wanaume 17 na wanawake 25—pamoja na wafanyakazi wa ziada kama walezi, wapishi, walinzi na katibu.
Mradi wa EACOP) una kilomita 1,443 kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale, Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.
Mradi huo unamilikiwa kwa ubia na TotalEnergies (62%), Uganda National Oil Company (15%), Tanzania Petroleum Development Corporation (15%), na CNOOC (8%).





