Breaking News

BRELA YASISITIZA ULINZI WA BUNIFU ZINAZOFANYWA JESHINI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umesisitiza umuhimu wa taasisi za kijeshi kusajili na kulinda bunifu zinazozalishwa ndani ya Jeshi ili kuhakikisha zinapata ulinzi wa kisheria na kuendelea kuchochea maendeleo ya teknolojia na ubunifu nchini.

Hayo yameelezwa leo tarehe 15 Mei, 2026 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa alipofanya mazungumzo na wawakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzinga katika ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam na kuwakabidhi tuzo yao ya Ubunifu Bora wa Mwaka 2026 waliyoipata siku ya maadhimisho ya Miliki Ubunifu Duniani hivi karibuni.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Nyaisa alisema bunifu nyingi zinazotengenezwa ndani ya Jeshi zina thamani kubwa na ya kipekee, hivyo ni muhimu zaidi kulindwa ili kuzuia watu wengine kuziiga au kuzisajili kwa maslahi yao binafsi.
Inawezekana mkawa na teknolojia au formula ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuitengeneza, lakini kama haijasajiliwa mtu mwingine anaweza kunakili na kwenda kuisajili na akaonekana ndiye mmiliki, kumekuwa na changamoto baadhi ya wabunifu kupoteza haki zao kwa kutosajili mapema kazi zao.” Alisema Bw. Nyaisa. 

Aidha, Bw. Nyaisa ameeleza kuwa BRELA ipo tayari kutoa elimu kuhusu usajili wa bunifu, ulinzi wa hataza na haki za miliki ubunifu kwa taasisi mbalimbali za jeshi huku akizihimiza taasisi za utafiti ndani ya Jeshi kuendelea kufanya tafiti na kubuni teknolojia zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kupitia suluhisho za kisasa na bunifu.

“Mataifa mengi yaliyoendelea yamefanikiwa kwa kuwekeza katika ulinzi wa miliki bunifu na hataza, mfano nchi kama China wana bunifu nyingi ambazo zimelindwa na zinachangia kukuza uchumi wa nchi yao na kuhimili ushindani na mataifa mengine ndiyo maana hata sisi tunasisitiza kufanya mambo kisayansi na kuhakikisha bunifu zote zinasajiliwa na kulindwa” alisisitiza Bw. Nyaisa. 
Kwa upande wake, Captain William Gissila Gurtu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzinga Brigedia Jenerali Seif Athuman Hamis aliishukuru BRELA kwa elimu iliyotolewa na kueleza kuwa imepata uelewa mkubwa zaidi kuhusu umuhimu wa kulinda bunifu huku akisema kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili utaendelea kuimarishwa zaidi.

Shirika la Mzinga Morogoro lilitunukiwa tuzo ya Ubunifu Bora wa Mwaka 2026 kwa kutambua mchango wake katika ubunifu, tafiti na maendeleo ya teknolojia mbalimbali zinazosaidia sekta ya ulinzi pamoja na jamii kwa ujumla baada kutengeneza bomu baridi la kufukuza tembo kwenye makazi ya watu bila ya kuleta madhara kwa tembo, binadamu na mazingira.