Breaking News

WANAWAKE WAJASIRIAMALI WAPEWA RUNGU UBALOZI HAMASA ULIPAJI KODI KWA HIARI

Na Mashaka Kibaya, TANGA - Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utoaji wa elimu ya kodi na huduma kwa walipakodi, baada ya kuwataka wanawake wajasiriamali kutumia nafasi zao katika jamii kuwa mabalozi wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.

Wito huo umetolewa na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, wakati akifungua Jukwaa la Wanawake na Kodi lililoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali kuhusu masuala ya kodi na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika mfumo rasmi wa uchumi.

Akizungumza katika tukio hilo, alisema jukwaa hilo limekuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wanawake wajasiriamali na TRA, kwa kuwapa elimu sahihi ya kodi, kuwasaidia kujiunga na mifumo ya kodi pamoja na kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kwa hiari na kwa wakati.
“Wanawake wajasiriamali wana nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi. Wakisimama imara katika kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, wanakuwa sehemu ya moja kwa moja ya maendeleo ya taifa,” alisema Castro.

Aliongeza kuwa TRA itaendelea kuboresha huduma zake na kuweka mazingira rafiki kwa walipakodi, huku akisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuepuka biashara zisizo rasmi zinazopitishwa kwa njia zisizo halali maarufu kama ‘njia za panya’, kwani huikosesha Serikali mapato muhimu kwa maendeleo ya wananchi.

Aidha, aliwahimiza wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa au huduma mbalimbali ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, huku akisisitiza kuwa milango ya TRA ipo wazi kwa huduma na ushauri kwa wafanyabiashara wote.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Ismail Masudi, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kukwepa kodi, akieleza kuwa kadri idadi ya walipakodi inavyoongezeka ndivyo inavyorahisisha kubaini wanaokwepa na hivyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Naye Kaimu Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Charles Mkumbwa, alisema jukwaa hilo ni mkakati mahsusi wa kuwafikia wanawake wajasiriamali na kuwajengea uelewa kuhusu nafasi yao katika kukuza uchumi wa taifa kupitia ulipaji kodi.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga, Charles Mtali, alisema wanawake ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi, akibainisha kuwa kuwawezesha kwa elimu ya kodi kutachochea zaidi mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Jukwaa la Wanawake na Kodi limeendelea kuwa chachu ya mabadiliko, likijenga uelewa, utii wa kodi kwa hiari na ushirikiano imara kati ya TRA na wanawake wajasiriamali hatua inayodhihirisha mafanikio ya wazi katika safari ya kujenga uchumi jumuishi na endelevu nchini.