Breaking News

JOWUTA YATOA WITO WANAHABARI KUJIUNGA KWA ULINZI WA MASLAHI YAO

Dar es salaam - Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimetoa wito kwa wanahabari nchini kuhakikisha wanajiandikisha katika chama hicho ili kuimarisha ulinzi wa maslahi na stahiki zao mahala pa kazi.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma Siwayombe, wakati akizungumza katika kikao kazi cha WCF na JOWUTA kilichowakutanisha zaidi ya waandishi wa habari 90 kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kilichofanyika leo Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam.
Siwayombe amesema bado wanahabari wengi wanafanya kazi bila ajira za kudumu, hali inayowaathiri kushindwa kupata huduma muhimu za hifadhi ya jamii pamoja na fidia wanapopatwa na madhara kazini.

Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wanahabari nchini hawana ajira rasmi, jambo ambalo linaendelea kuathiri ustawi wa tasnia ya habari na maisha ya waandishi wengi.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema ni muhimu kwa wanahabari kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani ndiyo njia ya kujenga umoja pamoja na kulinda na kutetea haki zao mahala pa kazi.

Nyamhokya amesema waandishi wengi wanafanya kazi katika mazingira hatarishi bila mikataba rasmi kutoka kwa waajiri wao, hali inayowafanya kukosa uhakika wa maisha na mafao yao pale ajira zinapositishwa.
“Vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na kutetea maslahi yao wanapokumbwa na changamoto kazini. Hivyo, natoa wito kwa waandishi wa habari kujiunga na chama hiki ili kuwepo sauti ya pamoja katika mapambano ya kutetea haki na maslahi yao,” amesema Nyamhokya.

Kikao kazi hicho kililenga kuongeza uelewa kwa wanahabari kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi pamoja na kuwajengea maarifa kuhusu haki na stahiki zao kupitia vyama vya wafanyakazi ikiwemo JOWUTA.