Breaking News

UFARANSA YATOA MILIONI 35 KUIMARISHA KILIMO IKOLOJIA TARIME

Na Mwandishi Wetu - UBALOZI wa Ufaransa kupitia Mradi wa Agro Kilimo unaoratibiwa na Shirika la Island of Peace (IDP), umekipatia Kituo cha Maendeleo ya Kilimo na Mazingira Mogabiri (MFEC) shilingi milioni 35 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umwagiliaji wa mazao yanayolimwa kwa mbinu za kilimo ikolojia.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa MFEC, Peter Mwita, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho kilichopo wilayani Tarime, mkoani Mara.

Mwita amesema Mradi wa Agro Kilimo umeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa kituo hicho kupitia kubadilishana uzoefu na wadau wa kilimo ikolojia pamoja na kupokea msaada wa miundombinu inayosaidia kuendeleza mashamba darasa kwa ajili ya wakulima wa Tarime.

“Ubalozi wa Ufaransa kupitia IDP umetupatia msaada wa shilingi milioni 35 ambazo zimetumika kujenga jengo la kuweka matangi mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita 20,000 za maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba ya mfano wakati wa ukame au kipindi cha jua,” amesema Mwita.

Amesema kupitia msaada huo, MFEC inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kilimo ikolojia na matumizi ya umwagiliaji katika kuongeza uzalishaji.
Mwita amesema matarajio yao ni kuona wakulima wa Tarime na Tanzania kwa ujumla wakijikita katika kilimo ikolojia kutokana na uwezo wake wa kuzalisha chakula salama na rafiki kwa afya ya mlaji.

Amesema wakulima wengi wa Tarime na Mkoa wa Mara watanufaika na mradi huo, jambo linalowapa nguvu ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

“MFEC Mogabiri tunazalisha mazao mbalimbali kwa njia ya kiikolojia ikiwemo migomba, sukuma wiki, nyanya, hoho, kabichi, viazi na muhogo. Tunawaomba wakulima wajitokeze kwa wingi kujifunza,” amesema.

Aidha, amesema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1986 pia kinafuga mifugo inayosaidia uzalishaji wa mbolea ya samadi na mboji.

Mwita amesema MFEC imekuwa ikitoa mafunzo ya utengenezaji wa viuatilifu vya asili kwa wakulima wanaofika kujifunza kituoni hapo.
Kwa mujibu wa Mwita, kituo hicho tayari kimefikia zaidi ya wakulima 35,000 kutoka vijiji 33 vya wilaya ya Tarime na sasa kimeanza kupokea maombi ya mafunzo kutoka nje ya Mkoa wa Mara.
Hata hivyo, amesema juhudi za kuhamasisha jamii kujikita katika kilimo ikolojia bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa rasilimali za asili na sera ambazo hazihamasishi vya kutosha matumizi ya kilimo hicho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa IDP, Ayesiga Buberwa, amesema Mradi wa Agro Kilimo ni mwendelezo wa kampeni ya kuhamasisha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula.

Amesema uzalishaji wa chakula kuanzia shambani hadi mezani unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo MFEC.

“Mradi huu umejikita katika mafunzo na tafiti zitakazowezesha wakulima kujikita zaidi katika kilimo ikolojia. Tunashukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kufadhili eneo hili muhimu kwa afya ya binadamu,” amesema Ayesiga.

Ameongeza kuwa mradi huo umewezesha vituo mbalimbali vya kilimo ikolojia kushirikiana, kutoa mafunzo kwa wakulima na kuboresha miundombinu ya ukusanyaji wa maji kwa matumizi ya muda mrefu.

Ayesiga ametaja vituo vingine vilivyopo kwenye mradi huo kuwa ni pamoja na SJS Mwanga, RECODA, Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Bihawana Dodoma na PPIZ Zanzibar.
Naye Mwakilishi wa Serikali ya Ufaransa, Profesa Jean Luc Paul, amesema nchi hiyo imeendelea kutoa msaada katika sekta ya kilimo nchini Tanzania kwa lengo la kusaidia wakulima kuzalisha mazao kwa njia ya kiikolojia.

Profesa Jean Luc amesema Ufaransa imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya sekta ya kilimo Tanzania tangu mwaka 1980, hasa kupitia ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Amesema Ubalozi wa Ufaransa ulivutiwa na mikakati ya kuendeleza kilimo ikolojia na unaamini mradi huo utaleta mageuzi chanya kwa vituo vya kilimo na wakulima kwa ujumla.

“Mradi huu wa Agro Kilimo utawezesha mageuzi kwa wakulima na wasimamizi wa vituo hivi sita,” amesema.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake mzuri, akieleza kuwa hali hiyo inawapa matumaini kwamba siku moja kilimo ikolojia kitakubalika na kupewa kipaumbele na jamii nzima