Breaking News

MCHUNGAJI MSHUMBUSI AWATAKA VIJANA KUENZI UZALENDO NA KULINDA MALI ZA UMMA”

Mchungaji wa Kanisa la Jerusalem Assembly of God, Peter Mshumbusi, ambaye pia ni mwanajeshi mstaafu aliyeshiriki katika vita vya Kagera, amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kuwa wazalendo na kuipenda nchi yao.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa uzalendo, Mchungaji Mshumbusi amesema hata wakati wa vita walisisitizwa kulinda utu, nidhamu na kuheshimu mali za raia wa nchi jirani.

Amesema walipoingia nchini Uganda, viongozi wao waliwaelekeza kuwa waendelee kuonesha uzalendo wa kweli kwa kuheshimu wananchi na mali zao.

"Kamanda wetu alituasa kuwa, pamoja na kuwa tupo vitani, tunapaswa kuheshimu wananchi wa Uganda na mali zao kama tunavyoiheshimu Tanzania. Kutoka Mtukula hadi Kampala, hakuna nyumba tuliyovunja. Watu waliokimbia vita waliporudi walikuta makazi yao salama. Huo ndio uzalendo wa kweli," amesema Mchungaji Mshumbusi.

Aidha, amewataka vijana kuepuka vitendo vya uharibifu wa mali za umma na kuthamini maendeleo yaliyopo nchini, akieleza kuwa mengi yamejengwa kwa juhudi za wazalendo waliotangulia.