Breaking News

UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA ULIVYOTUMIKA KUCHOCHEA VURUGU ZA UCHAGUZI WA 2025

Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imefichua kuwa ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha uliwakabili vijana wengi, ulikuwa mwanya mkubwa uliotumiwa na baadhi ya watu kuwashawishi kushiriki katika ghasia na uharibifu wa miundombinu.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Tume na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, alibainisha kuwa changamoto za kijamii na kiuchumi zilizodumu kwa muda mrefu zilitengeneza mazingira hatarishi yaliyowafanya baadhi ya vijana, wakiwemo waendeshaji bodaboda na vijana wa mitaani wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi, kushawishiwa kirahisi kuingia barabarani.

Ushahidi uliokusanywa na tume hiyo unaonesha kuwa baadhi ya vijana waligeuzwa kuwa nguvukazi ya ghasia kwa kupewa kiasi kidogo cha fedha, kati ya Sh 10,000 hadi 50,000, ili kufanya fujo, kuchoma matairi na kuvuruga uchaguzi. Jaji Othman alisisitiza kuwa suala la ajira kwa vijana si suala la kiuchumi tu, bali sasa limekuwa ni suala la usalama wa taifa na utulivu wa kijamii, kwani vijana wanapokosa matumaini ya kesho hugeuka kuwa silaha ya kisiasa na kihalifu.

Ripoti hiyo pia limeeleza umuhimu wa kuwekeza katika sera za vijana, huku ikiongeza uzito katika jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Ripoti hiyo imeonesha kuwa uwekezaji katika sekta za uzalishaji si tu unaleta maendeleo, bali ni mkakati mkuu wa kulinda amani ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ambayo zaidi ya nusu ya wananchi wake ni vijana, inahitaji kuongeza nguvu katika kutoa elimu ya ujuzi, ufundi, teknolojia, na uwezeshaji wa kiuchumi. Hatua hii inaendana na msisitizo wa hivi karibuni wa Rais Samia katika kuwekeza kwenye sekta zinazozalisha ajira kwa wingi kama vile kilimo cha kisasa (BBT), viwanda, uchumi wa kidijiti na ujasiriamali.

Tume imebainisha kuwa ili kuzuia makundi yenye misimamo mikali na migogoro ya baadaye, serikali haina budi kutumia mafunzo ya ripoti hiyo kuimarisha mifumo ya mikopo na kupanua fursa za ajira. Ripoti inahitimisha kuwa taifa lenye vijana wenye matumaini na fursa za kiuchumi, huwa na uwezekano mdogo sana wa kushawishiwa kuingia kwenye maandamano ya hasira au uharibifu wa mali.