Breaking News

THE INTERNATIONAL EYE HOSPITAL YAZINDUA HUDUMA MPYA YA SMART LENS KWA WAGONJWA WA MACHO

Daktari Bingwa wa Macho wa The International Eye Hospital, Zayd M Sangey akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya Smart Lens, inayomwezesha mgonjwa kuona vitu vya karibu, vya kati na vya mbali kwa ufanisi mkubwa zaidi, hali inayosaidia kupunguza utegemezi wa matumizi ya miwani kwa baadhi ya wagonjwa, mapema leo Mei 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
Meneja Masoko wa The International Eye Hospital, Ally Chillo akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu huduma mpya ya Smart Lens wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.


Dar es salaam - Hospitali ya The International Eye Hospital imezindua rasmi huduma mpya ya Smart Lens, teknolojia ya kisasa inayolenga kuwasaidia wagonjwa wa macho kuona kwa ubora zaidi ikilinganishwa na lenzi za kawaida zilizokuwa zikitumika hapo awali.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Macho wa hospitali hiyo, Zayd M Sangey amesema kuwa Smart Lens inamwezesha mgonjwa kuona vitu vya karibu, vya kati pamoja na vya mbali kwa ufanisi mkubwa zaidi, hali inayomsaidia kuondokana na utegemezi wa matumizi ya miwani kwa baadhi ya wagonjwa.

Dkt. Sangey amesema huduma hiyo ni suluhisho muhimu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho, ambao kwa kiasi kikubwa husababishwa na mabadiliko ya umri pamoja na mabadiliko ya mtindo wa maisha. Ameeleza kuwa magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na mafuta mengi mwilini huongeza kasi ya kupata ugonjwa huo.

“Huduma hii mpya ya Smart Lens inamwezesha mgonjwa kuona karibu, kati na mbali. Kwa wagonjwa ambao hawataki kuendelea kutumia miwani mara kwa mara, huduma hii inaweza kuwa suluhisho bora zaidi,” amesema Dkt. Sangey.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa hospitali hiyo, Ally Chillo amesema wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo watapitia uchunguzi wa awali wa macho kabla ya kufanyiwa matibabu hayo.

Amefafanua kuwa mgonjwa atafanyiwa vipimo mbalimbali vya kitabibu ili kubaini kama macho yake yako tayari kwa kuwekewa lenzi hiyo maalumu.

“Tunawakaribisha wananchi kufika hospitalini hapa kwa ajili ya uchunguzi wa awali. Vipimo vitafanyika ili kujiridhisha kama mgonjwa anastahili kupata huduma ya Smart Lens au la,” amesema Chillo.

Uzinduzi wa huduma hiyo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya ya macho nchini, huku ukitoa matumaini mapya kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kisasa yenye matokeo bora zaidi ya kuona