WANAVYUO WAPAZA SAUTI, YALIYOTOKEA OKTOBA YASIJIERUDIE
Dar es salaam - Katika nyakati ambazo dunia inakabiliwa na changamoto za migawanyiko, chuki na vurugu, vijana wa Tanzania wameendelea kuonyesha dhamira ya kulinda tunu za taifa letu amani, umoja na mshikamano. Kauli mbiu ya “Never Again” imeendelea kupata nguvu kutoka kwa vijana wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wakisisitiza kuwa Tanzania haitakiwi kurudi katika mazingira yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 16, 2026 katika kongamano la wanafunzi wa vyuo lililofanyika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba amesema wanavyuo wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaunga mkono tamko la “Never Again” lililotolewa na vijana wa Mkoa wa Dodoma mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kongamano hilo lililoandaliwa na TAHLISO Mkoa wa Dar es Salaam chini ya kauli mbiu “Never Again – Tuipende, Tuitunze, Tuilinde Nchi Yetu” lilikuwa jukwaa muhimu kwa vijana kujadili nafasi yao katika kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Kiliba alisema msingi wa kongamano hilo unatokana na ujumbe uliotolewa na vijana wa Dodoma mbele ya Rais Samia, ambapo walisisitiza kutokuwa tayari kushirikiana na mtu au kundi lolote lenye nia ya kuvunja misingi ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini. Aidha, vijana hao walitoa msisitizo kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 29 hayapaswi kujirudia tena.
Kwa mujibu wa Kiliba, vijana wa vyuo wana wajibu mkubwa wa kuwa walinzi wa maadili ya taifa na kuhakikisha elimu wanayoipata inatumika kujenga jamii yenye mshikamano badala ya migawanyiko. Amesema kizazi cha sasa kina nafasi ya kipekee ya kuendeleza historia ya Tanzania kama taifa lililojengwa juu ya misingi ya upendo, kuheshimiana na uzalendo.
Kauli ya “Never Again” imeonekana kuwa si maneno ya kawaida kwa vijana hao, bali ni tamko la kizalendo linalobeba dhamira ya kuhakikisha amani ya Tanzania inalindwa kwa nguvu zote. Kupitia makongamano kama hayo, vijana wanaendelea kuhamasishwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda utulivu wa nchi na kuenzi urithi wa taifa uliodumu kwa miongo mingi.




