WANNE MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MWANAFUNZI WA IFM
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya James Rogers Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).
Watuhumiwa hao ni Steven Rogers Chaka (31), Afisa Maabara na mkazi wa Bomang’ombe, Hai mkoani Kilimanjaro; Anna Frank Lema maarufu kama Happines (30), mfanyabiashara mkazi wa Tabata Chang’ombe; pamoja na Twalibu Khamis maarufu kama Mputo (23) na Michael John maarufu kama Tambali (26), wote wakazi wa Kigogo Kati jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa polisi, kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na uchunguzi wa kina kufuatia tukio hilo la kusikitisha, ambapo mwili wa marehemu ulipatikana ukielea kwenye maji ya Mto Msimbazi, eneo la Kipawa Ilala, Aprili 30, 2026, ukiwa hauna kichwa.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa bado linaendelea na uchunguzi, likiwemo uchambuzi wa vielelezo vilivyokusanywa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za kisheria zikiendelea, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika, kwa mujibu wa ushahidi utakaopatikana.




