MAJALIWA KUONGOZA TAMASHA LA TANZANIA YA THAMANI KUIBUA FURSA KWA VIJANA
Vijana wabunifu na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam katika Tamasha la Tanzania ya Thamani, jukwaa linalolenga kuibua fursa za biashara, ubunifu na maendeleo kwa vijana.
Tamasha hilo litafanyika Juni 19, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, likiwa na dhamira ya kuwaunganisha vijana, kuhamasisha uzalendo na kukuza fursa za kiuchumi kupitia sanaa, teknolojia na ubunifu.
Mgeni rasmi katika tamasha hilo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu mstaafu na Mshauri wa Rais katika Masuala ya Kijamii, Kassim Majaliwa, ambaye ataongoza kongamano hilo litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo, sekta binafsi na vijana wajasiriamali.
Mbali na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu, tamasha hilo pia litatoa nafasi za mitandao ya kibiashara, ajira na mafunzo kwa vijana, huku washiriki watakaobuni mawazo bora ya biashara wakitarajiwa kutunukiwa zawadi mbalimbali.
Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo, Malick Sangura amesema kutakuwa na shughuli mbalimbali za ubunifu, ikiwemo mashindano ya uchoraji, mitindo, sarakasi na ngoma za asili.
Aidha, tamasha hilo litapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, akiwemo Jose Chameleone, hatua inayotarajiwa kuongeza mvuto na ushiriki wa vijana katika tukio hilo.




