Breaking News

SERIKALI YAENDELEA KUENDELEZA MAENEO MAALUM YA UWEKEZAJI KUVUTIA WAWEKEZAJI

Serikali imesema inaendelea kutekeleza mkakati wa kutenga, kulipa fidia na kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji (SEZ) kwa lengo la kuvutia wawekezaji, kuongeza shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Itigi, Yohana Stephen Msita, kuhusu mkakati wa Serikali wa kutenga maeneo hayo na kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha uwekezaji.

Dkt. Chaya amesema kuwa kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Serikali inaendelea kushirikiana na wizara, taasisi za umma na wadau mbalimbali kutambua maeneo ya kimkakati, kuandaa mipango kabambe, kufanya upembuzi yakinifu na kuweka miundombinu muhimu kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema hadi Mei 2026, jumla ya maeneo 34 maalum ya kiuchumi yalikuwa yametangazwa rasmi nchini. Kati ya hayo, maeneo 16 yako chini ya usimamizi wa TISEZA, maeneo 12 yanamilikiwa na sekta binafsi, manne yanamilikiwa na halmashauri za serikali za mitaa na mawili yanamilikiwa na taasisi za umma.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuyatafutia maeneo hayo wawekezaji ili yaweze kuanza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na utoaji wa ajira kwa wananchi.

Sambamba na hilo, Serikali imeziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yanalindwa dhidi ya uvamizi na migogoro ya ardhi.

“Serikali inazihimiza halmashauri kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, yakiwemo yaliyolipwa fidia na yale yanayosubiri kulipwa fidia, yanalindwa kikamilifu ili kuzuia uvamizi na kupunguza migogoro ya ardhi,” amesema Dkt. Chaya.