Breaking News

TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHA UTABIRI WA HALI YA HEWA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA ZA KISASA

Arusha - Serikali ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa na huduma za tahadhari za mapema kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence-AI) na Machine Learning, ili kulinda maisha, mali na kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Akifungua rasmi Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuhusu Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kiutendaji (Operational Climate Prediction-OCP4) unaofanyika jijini Arusha, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo mafuriko, ukame na vimbunga.

Profesa Mbarawa alisema ni heshima kubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu ulipoanzishwa mwaka 2015, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha nafasi inayozidi kuongezeka ya Afrika katika mijadala ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Aliwataka wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kutumia mkutano huo kujadili mbinu za kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa kuzingatia maendeleo ya kisayansi, mifumo ya ukusanyaji wa takwimu na matumizi ya teknolojia mpya ili taarifa zinazozalishwa ziweze kusaidia kufanya maamuzi sahihi kwa wakati.

Profesa Mbarawa alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa kwa kuongeza vituo vya uchunguzi, rada za hali ya hewa, kituo cha kitaifa cha ukarabati na uthibitishaji wa vifaa vya hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya utabiri na mafunzo kwa wataalamu.

Alieleza kuwa kupitia ushirikiano na WMO pamoja na wadau wa maendeleo, Tanzania inaendelea kutekeleza programu za Systematic Observation Financing Facility (SOFF) na Early Warnings for All zinazolenga kuboresha uchunguzi wa hali ya hewa, utabiri wa hali ya hewa na huduma za tahadhari za mapema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Millya, alisema Tanzania inauthamini ushirikiano wake wa muda mrefu na WMO tangu ilipojiunga na shirika hilo mwaka 1962.

Alisema ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya huduma za hali ya hewa nchini kupitia uhamishaji wa teknolojia, mafunzo ya wataalamu, misaada ya kitaalamu na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Millya alisema Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuimarisha huduma za hali ya hewa, mifumo ya tahadhari za mapema na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Athari za Maafa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang'a, alisema mkutano huo umefanyika wakati mahitaji ya taarifa sahihi, zinazotegemewa na zinazoweza kutumika katika kufanya maamuzi yanaongezeka, hasa kwa jamii zinazotegemea shughuli zinazochangiwa na hali ya hewa.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Bi. Ko Barrett, alisema matumizi ya teknolojia za Akili Unde yana uwezo wa kutoa utabiri wa hali ya hewa wenye ubora wa juu kwa gharama ndogo za kiuhesabu, hatua itakayowezesha mataifa mengi zaidi kuzalisha utabiri wao na kutoa tahadhari za mapema zinazookoa maisha ya watu.

Mkutano huo wa siku kadhaa umewakutanisha wataalamu wa hali ya hewa, watafiti, watunga sera, vituo vya kikanda na kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha huduma za utabiri wa hali ya hewa duniani.