Breaking News

ACT WAZALENDO YAIKOSOA SERIKALI UTEKEREZAZAJI BIMA YA AFYA KWA WOTE

DAR ES SALAAM – Chama cha ACT Wazalendo kimekosoa utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya, kikidai kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote bado haujawafikia wananchi wengi, hususan wenye kipato cha chini.

Tathmini hiyo imetolewa leo, Agosti 27, 2026, na Waziri Kivuli wa Afya na Ustawi wa Jamii wa ACT Wazalendo, Dkt. Elizabeth Benedict Sanga, ambaye amesema utekelezaji wa ahadi hizo umebaki na changamoto katika upatikanaji wa bima, huduma za kibingwa, dawa, vifaa tiba na watumishi wa afya.

Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, Serikali ilikuwa imeahidi ndani ya siku 100 kuzindua Bima ya Afya kwa Wote, kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo wenye magonjwa sugu, kuajiri watumishi wa afya 5,000 na kukomesha utaratibu wa kuzuiwa kwa miili ya marehemu hospitalini kutokana na madeni ya matibabu.

ACT Wazalendo inadai kuwa hadi sasa watu 997,015 pekee ndio walikuwa wamesajiliwa katika Bima ya Afya kwa Wote, huku 501,981 kati yao wakiwa bado hawajapatiwa kadi. Chama hicho kinasema hali hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wanaoishi katika mazingira ya umaskini, hivyo kasi ya utekelezaji inaweza kuchukua muda mrefu kuwafikia walengwa.

Chama hicho pia kimekosoa mfumo wa vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote, vikidai kuwa madaraja ya Ngorongoro Afya, Mikumi Afya, Serengeti na Tanzanite Afya yanatofautiana kwa kiwango cha huduma kulingana na uwezo wa mwananchi kulipia.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, baadhi ya huduma muhimu za kibingwa, ikiwemo uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo, MRI na CT-Scan, hazijafikiwa kikamilifu na wananchi wenye uwezo mdogo, jambo ambalo ACT Wazalendo inasema linaweza kuathiri utekelezaji wa dhana ya bima inayolenga kuwafikia wananchi wote.

Aidha, ACT Wazalendo imesema ahadi ya Serikali ya kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo wenye magonjwa sugu haijatekelezwa kwa kiwango kilichoahidiwa.

Katika suala la watumishi wa afya, chama hicho kimesema mahitaji ya watumishi nchini yanafikia 348,923, huku waliopo wakifikia takribani 182,430, sawa na asilimia 52.3 ya mahitaji hayo. Kwa makadirio yake, Serikali ingehitaji kuajiri wastani wa watumishi 33,298 kwa mwaka ndani ya miaka mitano ili kufikia mahitaji yaliyopo.

ACT Wazalendo pia kimeibua suala la dawa na vifaa tiba, kikidai kuwa wananchi wenye bima bado hukumbana na changamoto za upatikanaji wa dawa, vifaa na vipimo, huku madeni ya Serikali kwa Bohari ya Dawa (MSD) yakitajwa kufikia takribani Sh471.11 bilioni.

Kuhusu ahadi ya kukomesha kuzuiwa kwa miili ya marehemu hospitalini kutokana na madeni ya matibabu, ACT Wazalendo imesema bado kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya familia zinazodaiwa kutakiwa kulipa madeni kabla ya kukabidhiwa miili ya ndugu zao.

Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa Wote unaounganishwa na Bima ya Afya, ambapo wananchi wa sekta rasmi na isiyo rasmi watachangia kulingana na uwezo wao, huku Serikali ikigharamia asilimia 100 ya huduma kwa wananchi wasio na uwezo.

Chama hicho pia kimetaka kila mwanachama awe na bima moja yenye huduma sawa na inayogharamia magonjwa muhimu, pamoja na Serikali kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini ili kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje.

ACT Wazalendo imesema mapendekezo hayo yanalenga kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inakuwa mfumo unaowezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila kutegemea uwezo wao wa kifedha.

Tathmini hiyo imetolewa na Dkt. Elizabeth Benedict Sanga, Waziri Kivuli wa Afya na Ustawi wa Jamii wa ACT Wazalendo, kwa lengo la kueleza msimamo wa chama hicho kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia katika sekta ya afya.