Breaking News

WATU 11 MBARONI KWA TUHUMA ZA KUHUJUMU MIUNDOMBINU YA TTCL

DAR ES SALAAM – Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata na kuwashikilia watu 11 kwa tuhuma za wizi, uharibifu na uhujumu wa miundombinu ya mawasiliano ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam leo Agosti 27, 2026 Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kati ya Juni, Julai na Agosti mwaka huu.

Polisi imeeleza kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao ni Timoth Emesho maarufu Jack na wenzake 10, waliokamatwa kwa kushirikiana na Kitengo cha Usalama cha TTCL.

Watuhumiwa hao walikutwa na baadhi ya nyaya za shaba (copper) zinazomilikiwa na TTCL, huku vifaa vilivyotajwa kutumika katika uhalifu huo vikijumuisha sururu, kofia ngumu, reflector, misumeno na nguzo.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya usalama katika Mitaa, Kata, Tarafa na Wilaya, likisisitiza umuhimu wa kuzuia vitendo vya uhalifu na uvunjaji wa sheria.

Aidha, Polisi imeonya kuwa haitamvumilia mtu yeyote atakayehusika katika hujuma dhidi ya miundombinu ya TTCL, iwe kwa kupanga, kuiba, kusafirisha au kupokea mali zinazohusiana na miundombinu hiyo.

Jeshi hilo pia limewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuwafichua wahalifu na kuahidi kuendelea kulinda miundombinu ya Taifa, watu na mali nyingine halali.