ACT WAZALENDO YAKOSOA UTITIRI WA BANDARI KAVU DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM - Chama cha ACT Wazalendo kimeibua hoja kuhusu ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, utitiri wa bandari kavu katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na malalamiko ya mawakala wa forodha kuhusu mfumo wa TCaMS, kikisema changamoto hizo zinaweza kuathiri mtiririko wa usafirishaji na shughuli za kiuchumi nchini.
Waziri Kivuli wa Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu wa ACT Wazalendo, Mtutura Abdalah Mtutura, amesema chama hicho kimeamua kufuatilia kwa karibu masuala hayo kutokana na umuhimu wa usafirishaji katika uchumi wa nchi, hususan katika Jiji la Dar es Salaam.
Mtutura amesema ACT Wazalendo imeangazia maeneo matatu muhimu, ambayo ni ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, ongezeko la bandari kavu ndani ya Jiji la Dar es Salaam na madhara yake kwa mipango miji, usafirishaji na gharama za biashara, pamoja na malalamiko ya mawakala wa forodha kuhusu mfumo wa TCaMS na namna mchakato wa kuanzishwa kwake ulivyofanyika.
Amesema chama hicho pia kitajikita katika kuchunguza masuala ya mtiririko wa mizigo kupitia bandari kavu, akieleza kuwa eneo hilo limeibua maswali na wasiwasi mbalimbali kuhusu ufanisi wa mfumo wa usafirishaji wa mizigo.
Kwa mujibu wa Mtutura, msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam unaohusishwa na shughuli za bandari kavu ni suala linalopaswa kuangaliwa kwa umakini kutokana na athari zake kwa mwendo wa wakazi na shughuli za kiuchumi.
Amesisitiza kuwa usafiri ni sehemu muhimu ya uchumi, akifananisha mtiririko wa magari na mishipa ya damu katika mwili wa binadamu.
Amesema pale ambapo mwendo wa magari unakwama au kutokuwa na ufanisi katika Jiji la Dar es Salaam, ambalo kwa mujibu wake linachangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la taifa, hali hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi.
Mtutura amesema ACT Wazalendo itaendelea kufuatilia masuala hayo, ikiwemo mapendekezo ya kisheria yanayohusu mfumo wa TCaMS, ili kubaini changamoto zilizopo na namna zinavyoweza kushughulikiwa.




