ACT WAZALENDO YAPINGA MADAI YA KUONGEZEKA KWA UFANISI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Dar es Salaam — Chama cha ACT Wazalendo kimepinga madai ya Serikali kwamba ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kufuatia uwekezaji mkubwa na kuanza kwa ubia na kampuni binafsi, kikisema baadhi ya viashiria vinaonyesha bado kuna changamoto katika utendaji wa bandari hiyo.
Akizungumza wakati akiwasilisha uchambuzi wa chama hicho kuhusu ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Kivuli wa Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu wa ACT Wazalendo, Mtutura Abdalah Mtutura, amesema ongezeko la shehena ya mizigo pekee haliwezi kutumika kama kipimo cha kuongezeka kwa ufanisi wa bandari.
ACT Wazalendo imesema shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam iliongezeka kutoka tani milioni 24.5 mwaka 2024 hadi takribani tani milioni 31.8 mwaka 2025. Hata hivyo, chama hicho kimesema ongezeko hilo lilikuwa sehemu ya mwenendo wa ukuaji wa shehena uliokuwepo kabla ya kuanza kwa ubia na kampuni ya DP World.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo, shehena katika bandari hiyo iliongezeka kutoka tani milioni 17 mwaka 2021 hadi milioni 19.9 mwaka 2022, milioni 22.9 mwaka 2023 na milioni 24.5 mwaka 2024, kabla ya kufikia tani milioni 31.8 mwaka 2025.
Chama hicho pia kimeibua hoja kuhusu utendaji wa Terminal 1, kikisema idadi ya makasha ya futi 20 yaliyohudumiwa ilipungua kutoka 212,268 mwaka 2024 hadi 179,701 mwaka 2025, sawa na kushuka kwa asilimia 15.3.
Aidha, ACT Wazalendo kimehoji muda ambao meli hukaa bandarini, kikisema wastani huo uliongezeka kutoka siku 3.8 mwaka 2021 hadi siku 9.6.
Chama hicho kimesema taarifa za mwaka 2024 zinaonyesha meli za makasha zilikaa bandarini kwa wastani wa siku 12.7, meli za shehena ya kawaida siku 13.7 na meli za mafuta siku 10.4.
Hoja kuhusu tozo ya PID
ACT Wazalendo pia imehoji kuendelea kutozwa kwa asilimia 4.5 ya Port Infrastructure Development (PID), ikitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu sababu za kuendelea kuwatoza watumiaji wa bandari fedha kwa ajili ya miundombinu wakati tayari kumefanyika uwekezaji mkubwa.
Chama hicho kimehoji pia namna mapato ya bandari yanavyogawanywa katika mazingira ambayo sehemu ya mapato inakwenda kwa mbia wa uendeshaji.
ACT Wazalendo yapinga ongezeko la bandari kavu
Katika hatua nyingine, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kudhibiti ongezeko la bandari kavu katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ikisema hali hiyo inachangia msongamano wa magari, kuchelewesha mizigo na kuongeza gharama za biashara.
Kwa mujibu wa chama hicho, hadi Machi 2025 kulikuwa na bandari kavu 90 zilizosajiliwa, zikiwemo CFA 35, ECD 13, ICD 21, ICDV 14 na ICD Silos saba.
ACT Wazalendo pia imehoji matumizi hafifu ya Bandari Kavu ya Kwala, ambayo Serikali imewekeza katika miundombinu yake kwa lengo la kupunguza msongamano wa mizigo ndani ya Dar es Salaam.
Chama hicho kimesema Kwala iko takribani kilomita 90 kutoka Bandari ya Dar es Salaam na imeunganishwa na reli ya MGR pamoja na barabara, hivyo inaweza kutumika kama eneo muhimu la kuhifadhi na kuhudumia mizigo.
ACT Wazalendo imependekeza Serikali isimamishe utoaji wa vibali vipya vya bandari kavu katikati ya jiji na kuandaa utaratibu wa kuhamisha zilizopo kwenda katika maeneo yaliyopangwa nje ya jiji, ikiwemo Kwala.
ACT Wazalendo yaitaka Serikali kusimamisha TCAMS
Kuhusu Trade and Customs Agents Management System (TCAMS) unaohusishwa na kampuni ya Capital Pay, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kusimamisha utekelezaji wa mfumo huo hadi mashauriano ya kina yafanyike kati ya vyama vya mawakala wa forodha na wanachama wao.
Chama hicho kimesema kimepokea malalamiko kuhusu mchakato wa kuanzishwa kwa mfumo huo, ikiwemo madai ya wanachama wa vyama vya mawakala wa forodha kutoshirikishwa vya kutosha katika maamuzi yanayohusu mkataba huo.
Pia ACT Wazalendo imesema kuna malalamiko kwamba mfumo huo unaweza kuhusisha makato ya hadi asilimia 25 kwa mizigo ya kawaida na hadi asilimia 50 kwa mizigo ya madini, ikidai kuwa hali hiyo inaweza kuongeza gharama za uendeshaji na hatimaye gharama kwa waagizaji.
Chama hicho kimeitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu msingi wa kisheria wa matumizi ya TCAMS, usalama na umiliki wa taarifa za biashara zitakazohifadhiwa kwenye mfumo huo, pamoja na uhusiano wake na mifumo rasmi ya Serikali, ikiwemo TANESW.
ACT Wazalendo pia imetaka mkataba kati ya Capital Pay na vyama husika uwekwe wazi, huku TAKUKURU ikifanya uchunguzi huru kuhusu mchakato wa kuingia katika mkataba huo.
Aidha, chama hicho kimezitaka TASAC, TPA na TRA kutoa ufafanuzi kuhusu utambuzi na utekelezaji wa mfumo huo.
ACT Wazalendo imesema itaendelea kufuatilia uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, matumizi na ongezeko la bandari kavu pamoja na utekelezaji wa mfumo wa TCAMS, huku kikisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa miundombinu ya biashara nchini.




