Breaking News

POLISI DODOMA YATUMIA MAONESHO YA NANENANE KUTOA ELIMU YA KUIMARISHA USALAMA

DODOMA: Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema limeimarisha ulinzi na usalama katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, huku likitumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na jeshi hilo.

Akizungumza katika banda la Jeshi la Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gilles Mroto, alisema hali ya usalama mkoani humo ni shwari na jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda amani kupitia doria, misako na operesheni mbalimbali.

Alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya maonesho ili kuhakikisha wananchi wanashiriki shughuli hizo kwa usalama na amani, huku akiwakaribisha kutembelea viwanja hivyo kujionea teknolojia na huduma mbalimbali zinazotolewa.

ACP Mroto alisema Jeshi la Polisi ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, kikiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria, kulinda amani, kupeleleza makosa ya jinai, kukamata wahalifu na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

Alieleza kuwa pamoja na jukumu la kulinda usalama, jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake ili kuongeza uelewa na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika vituo vya polisi.

Katika maonesho hayo, Jeshi la Polisi linatoa elimu kupitia vitengo mbalimbali ikiwemo Dawati la Chumba cha Mashtaka, Polisi Jamii, Polisi Mtandao, Kitengo cha Alama za Vidole, Uzuiaji na Udhibiti wa Madawa ya Kulevya, Usalama Barabarani, Polisi Mazingira, Madini na Utalii, Makosa ya Mtandao, Interpol, Kitengo cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STU), Kitengo cha Mbwa na Farasi, Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto pamoja na elimu kuhusu madhara ya umiliki haramu wa silaha na ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama.

Aidha, Kamanda huyo alisema maonesho hayo yamewakutanisha pia waganga wa tiba asili ambao wamepewa elimu ya kuzingatia sheria wanapotoa huduma zao na kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu wanaoweza kuwafikia wakitaka kujificha au kujikinga dhidi ya uhalifu walioufanya.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kutembelea mabanda ya Jeshi la Polisi na vituo vya polisi vilivyopo nchini ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa lengo la kuimarisha usalama, amani na utulivu wa jamii.