Breaking News

BoT, IFC WASAINI MAKUBALIANO KUPANUA MIKOPO KWA BIASHARA NDOGO

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini hati ya makubaliano (MoU) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (International Finance Cooperation – IFC), kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa mikopo na huduma za fedha kwa biashara ndogo na za kati nchini, zikiwemo zile zinazomilikiwa na wanawake kupitia uhamasishaji wa matumizi ya taarifa mbadala katika kufanya tathmini ya mikopo (promotion and adoption of alternative data for credit assessment). 

IFC ni taasisi ya Kundi la Benki ya Dunia (World Bank Group) ambayo inasimamia masuala ya sekta ya binafsi.

Hafla ya utiaji saini imefanyika tarehe 21 Septemba 2026 katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza katika hafla hiyo Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba amesema makubaliano haya ya ushirikiano yamekuja katika wakati muafaka ambapo Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo malengo yake kwa kiasi yanategemea uwezeshwaji wa sekta binafsi. 

“Jambo hili limekuja wakati muafaka, kwa sababu hivi karibuni tumeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yenye lengo la kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani unaotarajiwa kufikia thamani ya Dola za Marekani trilioni moja”. Alisema

“Katika safari hii, tunatarajia ushirikiano na mchango mkubwa kutoka IFC katika kufanikisha azma hiyo, hususan kwa kuzingatia kwamba asilimia 70 ya mafanikio hayo yanategemea mchango wa sekta binafsi”. Alieleza Gavana huyo. 
Gavana Tutuba alisistiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa biashara na uwekezaji, ili kuwawezesha washiriki wote katika sekta ya fedha kutumia fursa zilizopo na kuchangia kikamilifu katika kufikia malengo ya Dira hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa IFC Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Mary-Jean Moyo, alisema mradi huo utasaidia kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, hususan wanawake, na kufungua fursa zaidi za ukuaji wa biashara na ajira.

Alisema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya IFC ya kusaidia maendeleo ya sekta binafsi na kuchochea uwekezaji nchini.

“Tanzania ni kitovu muhimu cha Afrika Mashariki na soko la kimkakati kwa IFC. Kuwa na uongozi wa kikanda hapa Dar es Salaam kunadhihirisha dhamira yetu ya kuendelea kuongeza uwekezaji, kuimarisha sekta binafsi, na kukuza fursa za kiuchumi kwa Tanzania na ukanda mzima,” alisema Moyo.