BRELA YATOA NOTISI YA MWISHO KUFUTA KAMPUNI KWENYE REJISTA
DAR ES SALAAM: Msajili wa Kampuni ametangaza notisi ya mwisho ya nia ya kufuta kampuni zilizoorodheshwa kwenye Daftari/Rejista ya Kampuni, ikiwa ni hatua inayowapa wahusika muda wa siku 90 kuwasilisha pingamizi kabla ya hatua hiyo kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa umma
Iliyotolewa Septemba 9, 2026 na kusainiwa na Msajili Msaidizi wa Kampuni, Leticia J. Zavu imesema Notisi hiyo imetolewa chini ya kifungu cha 403(3) cha Sheria ya Kampuni, Sura ya 212, na inawahusu wakurugenzi, wanahisa na makatibu wa kampuni zilizoorodheshwa kwenye jedwali lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la Septemba 18, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo inafuatia notisi mbili za awali zilizotolewa na Msajili wa Kampuni, ambapo ya kwanza ilitolewa Juni 2, 2022 na ya pili Julai 13, 2022, zikiwaagiza kampuni zilizoorodheshwa kuthibitisha kama zinaendelea kufanya biashara.
Msajili amesema kampuni hizo zinapewa muda wa mwisho wa siku 90 kuanzia tarehe ya tangazo kuwasilisha pingamizi. Endapo hakutakuwa na pingamizi ndani ya muda huo, Msajili ataendelea na hatua za kuzifuta kampuni hizo kutoka kwenye Daftari/Rejista ya Kampuni.
Orodha iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali inaanza na kampuni kama 2m & K Lime Products Limited, 3m Consult Limited, 5-Emu Enterprises Company Limited, 683 Autospares And Hardware Limited na nyingine nyingi kutoka sekta mbalimbali.




