GST YATUMIA MAONESHO YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI KUTOA ELIMU YA JIOLOJIA NA MADINI
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST) imejipanga kutumia maonesho ya Biashara ya Afrika ashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuwaelimisha wananchi, wachimbaji, wawekezaji na wadau mbalimbali kuhusu huduma zinazotolewa katika sekta ya jiolojia na madini nchini.
Fundi Sanifu mkuu kutoka GST, Gideon Nshange amesema hayo wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda lao katika maonyesho ya Biashara ya Afrika Mashariki
Nshange amesema taasisi hiyo ipo chini ya Wizara ya Madini, inajihusisha na tafiti za jiosayansi, uchunguzi wa madini, uchambuzi wa sampuli pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau wa sekta ya madini, ujenzi na mazingira.
Amesema GST ina uwezo wa kufanya uandaaji na uchambuzi wa sampuli za miamba na madini, ikiwemo tafiti za uchenjuaji wa madini, uchunguzi wa sampuli za mazingira pamoja na vipimo vya udongo, kokoto na miamba kwa ajili ya shughuli za ujenzi
Pia inatoa huduma za jiofizikia na jiolojia, zikiwemo tafiti za umagnetiki, umeme, radiometriki, uzito wa mvuto na uchunguzi wa mashimo ya madini. Huduma hizo husaidia katika kutambua na kuchunguza uwepo wa rasilimali chini ya ardhi.
Aidha, GST inaonesha ramani ya madini ya Tanzania pamoja na sampuli za baadhi ya madini na vito vinavyopatikana nchini, jambo linalowapa wananchi fursa ya kufahamu zaidi utajiri wa rasilimali za madini uliopo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Amesema maonesho hayo yanakuwa fursa muhimu kwa GST kuwafikia wananchi moja kwa moja, hasa wachimbaji wadogo, wawekezaji na wafanyabiashara wa madini, kwa kuwa taasisi hiyo hutoa ushauri kuhusu kutambua aina na ubora wa madini pamoja na njia bora za uchenjuaji.





