Breaking News

MSAJILI HAZINA ATETA NA UONGOZI WA KAMPUNI YA BARRICK

Na Mwandishi wa OTR, Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Barrick Corporation, mwanahisa mwenza wa Twiga Minerals Corporation Limited (TWIGA), pamoja na uongozi wa TWIGA, kujadili maendeleo na masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa miradi inayosimamiwa na kampuni hiyo.

Mazungumzo hayo yalifanyika Jumanne, Septemba 1, 2026, wakati ujumbe wa Barrick ulipofanya ziara katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), jijini Dar es Salaam.

Ujumbe wa Barrick uliongozwa na Roelie Gey Von Pittius, Meneja wa Fedha wa Barrick kwa Afrika na Mashariki ya Kati, akiambatana na Candace Simpson, Meneja wa Kodi wa Afrika na Mashariki ya Kati; Melkiory Ngido, Meneja wa Barrick nchini Tanzania; na Judith Chambua, Meneja wa Kodi wa Barrick Tanzania.

Katika kikao hicho, Serikali, kupitia OTR, na Barrick, ambao ni wanahisa wenza wa TWIGA, walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na uendeshaji wa miradi ya uchimbaji wa dhahabu inayomilikiwa kwa ubia kupitia TWIGA.

Miongoni mwa miradi iliyojadiliwa ni pamoja na migodi ya North Mara na Bulyanhulu, pamoja na Buzwagi, ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kufungwa.

Uongozi wa TWIGA pamoja na wataalamu kutoka Barrick walishiriki katika kikao hicho kwa kutoa taarifa na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na uendeshaji wa miradi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mchechu alisema Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa miradi ya TWIGA, kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inaendelea kwa ufanisi, kuongeza uzalishaji na kuchangia zaidi katika uchumi wa Taifa.

Aidha, Bw. Mchechu alisisitiza kuwa sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na mapato ya Serikali, ikiwemo kupitia gawio linalotokana na uwekezaji wa Serikali katika kampuni za madini.

Bw. Mchechu alisema Serikali inathamini ushirikiano wake na Barrick na inaendelea kutumia uzoefu uliopatikana kupitia uhusiano huo katika kuimarisha sekta ya madini nchini.

“Tunauthamini sana mchango wa aina ya ushirikiano tulionao na Barrick,” alisema.

Alisema Barrick imekuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya sekta ya madini nchini na kwamba ushirikiano huo umeiwezesha Serikali kupata uzoefu katika kusimamia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.
Bw. Mchechu alisema Serikali inaendelea kufanya mashauriano na taasisi zinazohusika ili kuhakikisha masuala yanayohusu uwekezaji na shughuli za kampuni hiyo yanashughulikiwa kwa ufanisi na kwa uelewa wa pamoja.

“Katika masuala muhimu kama haya yanayomhusu mshirika muhimu katika biashara muhimu, ni lazima serikali izungumze kwa sauti moja,” alisema.

Alisema Serikali inalenga kujenga mazingira yatakayowezesha uwekezaji kuendelea kukua na kutoa manufaa ya muda mrefu kwa Tanzania.

“Tunataka kuwa na biashara ambayo inaweza kuendelea kwa utulivu kizazi hadi kizazi na kustahimili tawala mbalimbali za kisiasa,” alisema.

Kwa upande wake, Von Pittius alisema Barrick inaendelea kuthamini ushirikiano wake na Serikali na inaendelea kushirikiana na mamlaka husika katika masuala yanayohusu shughuli zake nchini.

Bw. Von Pittius alieleza nia ya kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa uwekezaji na maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Mazungumzo ya Jumanne ni sehemu ya mwendelezo wa ushirikiano kati ya Serikali na Barrick katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji na shughuli za madini nchini.