Kutoka Katavi: Atupwa Jela mwaka mmoja kwa kujiita Ripota Wa Star Tv Na Mtoto Wa Kamanda Kova.

Aliyekuwa akijita Ripota wa STAR TV
wa mkoa wa Katavi na mtoto wa Kamanda Suilemani Kova anayejulikana kwa jina la
Gerald Kova mkazi wa mkoa wa Mwanza amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela
baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya utapeli na kujipatia mali kwa njia
ya udanganyifu.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu
mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mpanda Marko Pagyo baada ya Mahakama kulidhika
na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Mwendesha mashtaka wa jeshi la Polisi
WP Salima alidai Mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo hapo
Februari 8 mwaka huu katika eneo la Hotel ya Madina Manispaa ya Mpanda.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo ambaye
alikuwa anajitambulisha kuwa ni mwakilishi wa STAR TV yenye Makao yake makuu
Mkoani Mwanza na ni mtoto wa Kamanda Selemani Kova alijipatia kwa njia ya
udanganyifu Kamera moja aina ya Canon yenye thamani ya Tshs 3,500,000/= ,Laptop
moja na stendi ya Kamera ya video mali ya Elias Mlugala.
Alisema mtuhumiwa baada ya kuwa
amejipatia mali hizo kwa njia ya udanganyifu aliondoka Mpanda na kutokomea
kusikojulikana huku akiwa ametapeli kamera nyingine Kibada aina ya Nikon
D 7,200 kwa Ernest mali ya Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Katavi
yenye thamani ya Tshs 4,900,000.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia
mahakama kuwa mshtakiwa baada ya kutokomea haikujulikana alikokuwa amekimbilia
mpaka hapo mwezi Agosti alipokamatwa huko Kahama mkoani Shinyanga na huko
alikuwa ajitambulisha kwa jina la Crispin Masawe na alikamatwa baada ya kufanya
utapeli mwingine wa kujipatia kwa njia ya udanganyifu Laptop moja ya mwandishi
wa habari wa Kahama.
Alidai kuwa baada ya kukamatwa
alifikishwa katika mahakama ya Mwanzo ya Kahama na kuhukumiwa kifungo cha miezi
mitatu au kulipa faini ya Tshs 100,000 hata hivyo hakuweza kulipa na alikwenda
gerezani.
Mwendesha mashtaka alieleza ndipo
Elias na Kibada walitoa taarifa kituo cha polisi cha Mpanda juu ya mtuhumiwa
wao kuhukumiwa kifungo hivyo walifanya utaratibu na waliweza kwenda Kahama na
kumlipia faini hiyo na kumtoa gerezani na kisha akawa chini ya ulinzi wa polisi
na aliweza kusafirishwa hadi Mpanda na ndipo alipofikishwa Mpanda na Polisi
alipoonyesha vifaa vyote ambavyo alikuwa amemuuzia mfanya biashara mmoja wa
huko Maji Moto Wilayani Mlele mkoani Katavi.
Mshtakiwa Gerald Kova katika utetezi
wake kabla ya kusomewa hukumu aliiomba Mahakama imwachie huru kwa kile
alichodai kuwa anasumbuliwa na magonjwa pia mama yake mzazi ni mgonjwa na
anamtegemea yeye.
Baada ya utetezi huo hakimu Paragyo
alisoma hukumu na kuamuru mshitakiwa atumikie kifungo cha mwaka mmoja jela na
pindi atakapotoka gerezani atatakiwa kulipa Tshs 800,000.
Mshitakiwa huyo anatarajiwa
kufikishwa tena mahakamani hapo kwa ajiri ya kesi ya pili inayomkabili ya
kujipatia kamera Nicon mali ya chama cha waandishi wa habari mkoa wa Katavi
ambapo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa.



