Viongozi Wa Taasisi Iliyotangaza Kutoa Mikopo Kwa Wanafunzi Wa Elimu Ya Juu Wakamatwa Kwa Utapeli

Viongozi wa Taasisi ya
Kusaidia Jamii (TSSF) ambayo ilitangaza kuwa inatoa mikopo ya elimu ya juu
wamekamatwa na polisi baada ya kugundulika kuwa ni matapeli.
Wakurugenzi hao
wamekamatwa jana Jumatatu jioni mara tu baada ya mkutano wa waandishi wa habari
na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wa kuelezea
kuhusu uchunguzi uliofanyika baada ya Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato
Chumi kuomba mwongozo bungeni.
Chumi alitaka ufafanuzi
kuhusu uhalali wa taasisi hiyo baada ya kutangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa
elimu ya juu kwa kulipa Sh 30 000 kama ada ya maombi ya kusajiliwa kuomba
mkopo.
Hata hivyo, Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali
haitambui taasisi hiyo na kuahidi kufanya uchunguzi.
Akizungumza leo Jumanne,
Ole Nasha amesema baada ya uchunguzi huo wamebaini kuwa taasisi hiyo haina
uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 ambao ilitangaza kutoa.
Amesema katika mahojiano
na taasisi hiyo viongozi hao walisema kuwa fedha za kuwakopesha wanafunzi hao
watazipata kutoka nje ya nchi baada ya kupeleka kiasi cha fedha.
Hata hivyo, amesema
mkataba wa taasisi hiyo na wafadhili hao unaonyesha kuwa wamefikia makubaliano
ya kufanya utafiti wa jinsi wanavyoweza kukusanya fedha na si kuwapa fedha kwa
ajili ya kutoa mikopo.
Amesema tayari taasisi
hiyo imekusanya fedha kwa wanafunzi 600 na imepeleka wanafunzi 198 katika vyuo
mbalimbali nchini kwa makubaliano ada zao wangelipa Desemba mwaka huu.
Hata hivyo, amesema
hakuna uthibitisho kama wana fedha kweli za kuwalipia wanafunzi hao ada ingawa
wanadai kuwa katika akaunti zao za benki wana fedha kati ya Sh 600 milioni na
700 milioni.
Amesema kufuatia hilo
wanaagiza vyombo vya dola kuchunguza jambo hilo na wakati wakifanya hivyo ni
marufuku kwa vyuo kuwapokea wanafunzi wanaopewa mikopo na taasisi hiyo.
Pia ameagiza akaunti zao
zote kufungiwa hadi hapo watakapomaliza uchunguzi sambamba na taasisi hiyo kutojihusisha
na shughuli yoyote.
Baada ya kumaliza mkutano
huo polisi kutoka makao makuu ya polisi waliingia ndani ya ukumbi wa mkutano na
kuwaeleza wako chini ya ulinzi.
Polisi hao mmoja akiwa na
sare na mwingine akiwa na nguo za kiraia waliwakamata na kuondoka nao.



