Uzinduzi Wa Wa Ripoti Ya Shirika La Human Rights Watch Wazuiwa Jijini Dar

Mamlaka nchini Tanzania imezuia
uzinduzi wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa wafanyakazi wanawake kutoka taifa hilo
wanaofanya kazi katika mataifa ya Uarabuni.
Shirika la Human Rights Watch limedai
katika matokeo yake kwamba wafanyikazi wa nyumbani kutoka nchini Tanzania
walikuwa wakibakwa, kuteswa na kulipwa mishahara duni na waajiri wao katika
mataifa ya Uarabuni.
Ripoti yenye kurasa 100 inayodai
kuteswa kwa wafanyikazi wa nyumbani wa Tanzania nchini Oman na muungano wa
mataifa ya Emirata UAE ilitarajiwa kutolewa leo kwa waandishi wa habari mbele
ya waathiriwa lakini hilo halikufanyika.
Katika hatua isiokuwa ya kawaida,afisa
mmoja kutoka shirika linalofadhiliwa na serikali la Sayansi na Teknolojia
COSTEC William Kindekete alifutilia mbali mkutano huo na waandishi wa habari ambao
ulikuwa unaelekea kuanza jijini Dar es Salaam akisema kuwa wanaharakati wa
shirika hilo la haki za kibinaadamu hawakufuata sheria katika kufanya utafiti
wao.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo
wa HRW unaonyesha kuwa takriban wanawake 50 walihojiwa wakati wa utafiti huo
ambao wanadai kwamba walilazimishwa kufanya kazi kwa kati ya saa 15 na 21 kwa
siku huku wakipokonywa pasipoti zao na waajiri wao punde tu walipowasili katika
mataifa hayo.
Ripoti hiyo ilibaini zaidi kwamba
zaidi ya nusu yao hawakulipwa huku wengine wakisema kuwa hawakulipwa kabisa na Wawili
kati ya watano walidai kupigwa mbali na kunyanyaswa kijinsia.
Ripoti hiyo ya HRW pia inasema kwamba
balozi za Tanzania katika eneo la Ghuba hazikutoa usaidizi wowote kwa
waathiriwa wakati walipotaka usaidizi.
Juhudi za kupata majibu kutoka kwa serikali
ya Tanzania hazikufanikiwa kwa kuwa maafisa wengi hawakuwa tayari kuzungumzia
swala hilo.
Source BBC



