NIMEFURAHI SANA KUONA MZEE MWINYI KATAFUTA MUDA KUJA KUNIPA POLE…TUNDU LISSU

Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya umri wa miaka 93 alionao Rais
mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi bado amediriki kufunga safari
kwenda kumtembelea na kumpa pole.
Lissu, ambaye ni
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa kauli hiyo muda mfupi
baada ya kutembelewa na Mzee Mwinyi katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya
ambako anaendelea na matibabu.
Lissu amelazwa
hospitalini hapo tangu Septemba 7 anakotibiwa akiuguza majeraha ya kushambuliwa
kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma akitokea kuhudhuria
mkutano wa Bunge.
Akizungumza na
Mwananchi jana kwa simu kuhusu kutembelewa na Mzee Mwinyi, mwanasheria huyo wa
Chadema pamoja na mke wake, Alice walisema wamefurahi kutembelewa na kiongozi
huyo.
“Nimefurahi sana
kwamba umri wote alionao wa miaka 93 si kidogo, ametafuta muda kuja kunipa pole
hospitalini ni kitu kizuri sana, ni ubinadamu mkubwa sana,”alisema Lissu ambaye
alionekana mwenye furaha.
Rais mstaafu Mwinyi
anakuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali waliomtembelea Lissu kwani
hivi karibuni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye alifika hospitalini hapo
kumjulia hali.
Mzee Mwinyi
akiambatana na mke wake na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya walifika
hospitalini hapo kumjulia hali mbunge huyo na picha zinawaonyesha wawili hao
wakizungumza huku nyuso zao zikiwa na tabasamu.
Na Ibrahim Yamola,



