UNESCO Yaonya Athari Za Mapinduzi Ya Kidigitali Katika Uhifadhi Wa Nyaraka.
Shirika La Elimu,
Sayansi Na Utamaduni La Umoja Wa Mataifa Tanzania (UNESCO) limeonya uwepo wa athari
zitokanazo na mapinduzi ya matumizi ya mfumo wa kidjitali katika kuhifadhi
nyaraka muhimu za serikali na sekta binafsi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Bw. Lusajo Mwaitekele wakati
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mawasiliano na Habari kutoka Tume ya Taifa ya
UNESCO Tanzania- NATCOM, Christina Musaroche, katika semina kuhusu masuala ya
uhifadhi wa taarifa kwa kutumia mfumo wa kidijitali iliyoandaliwa na tume hiyo.
“Urithi wa kidijitali unaohifadhiwa kwa ajili ya manufaa ya vizazi
vijavyo uko hatarini kupotea kutokana na kasi ya mabadiliko ya mfumo huo
yanayotokea mara kwa mara yasiyoepukika,” alisema Bw Mwaitekele.
Akizungumza katika semina hiyo, Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa
Dkt. Amandus Kweka amesema athari hizo zinatokana na mabadiliko ya mara kwa
mara ya utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki vinavyotumika kuhifadhi nyaraka
hizo ikiwemo simu na kompyuta.
“Serikali inahamasisha jamii ihamie
kwenye mfumo wa dijitali bila ya kuwa na mikakati ya kuhifadhi taarifa za
nyuma. Inatakiwa tuwe na maandalizi ya namna gani tunatunza taarifa muhimu ili
ziweze leta faida kwa vizazi vya baadae,” amesema
na kuongeza.
“Serikali na wadau mbalimbali wanatakiwa
kuwa na mikakati itakayoendana na kasi ya mabadiliko ya mfumo huo hasa katika
kuhifadhi taarifa muhimu katika vyombo vya kidijitali ikiwemo simu na
kompyuta”.
Naye
Mhifadhi kutoka Makumbusho ya Taifa, Flower Manase ameishauri jamii hasa
serikali na taasisi binafsi kubadili namna ya kuhifadhi taarifa zao kila mara
ili kukwepa usumbufu ikiwemo kupotea kwa taarifa zao za muhimu.



