IGP SIRRO: JESHI LA POLISI LIKO IMARA KWELI KWELI...WENYE NIA YA KUCHAFUA AMANI TUSILAUMIANE

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)
Simon Sirro amesema Jeshi lake liko imara kweli kweli katika kupambana na watu
wanaotaka kuleta uvunjifu wa amani nchini, huku akiwasii wanaotaka kuandamana
kuacha mara moja kwani kitakachowapata wasije kulaumiana.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo leo
Aprili 7, 2018 wakati akitoa salamu zake kwa Rais Dkt. Magufuli katika uwanja
wa Sheikh Amri Abeid uliopo mjini Arusha baada ya uzinduzi wa nyumba za askari
na kushuhudia maonesho ya utayari ya jeshi hilo katika kukabiliana na uhalifu.
"Mhe. Rais Magufuli Jeshi lako
la Polisi liko imara tena imara kweli kweli, kwa kupambana na watu wote
wanaotaka kuleta uvunjifu wa amani hapa nchini na kwa bahati nzuri wananchi
wapo pamoja na wewe Rais na Jeshi lako.
" Ila naomba nitoe ushauri wa
bure kwa wale wote wenye nia ya kuchafua amani ya nchi yetu , niwasihi waache
mara moja na kama wataona ushauri huo hauna maana basi baadae
tusilaumiane", amesema IGP Sirro.
Pamoja na hayo, IGP Sirro ameendelea
kwa kusema "upo uhamasishaji kwenye mitandao, na hili niseme naamini
wameshaandamana kwenye mitandao na wameshamaliza maandamano yao. Kwa hiyo la
msingi sana tujenge nchi yetu".
Kwa upande mwingine, IGP Sirro
amesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Februari mwaka 2018 kuna jumla ya
matukio ya jinai yaliyoripotiwa ni 96,363 ikilinganishwa na matukio 104,073
yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2017.



