Hii Hapa Barua Ya Kumnusuru Askofu Malasusa Yasomwa Makanisani

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani(DMP), walisomewa barua maalumu
kuhusiana na suala la Askofu wao, Dk. Alex Malasusa.
Kusomwa kwa barua hiyo jana kunatokana na
kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani kilichokutana
Jumatano iliyopita.
Barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa
Dayosisi hiyo, Godfrey Nkini, ilisomwa katika usharika mbalimbali za dayosisi
hiyo wakati wa matangazo.
Kwa mujibu wa barua hiyo, washarika
wametakiwa kufahamu kwamba Dk. Malasusa ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na
Pwani na dayosisi itaendelea na umoja na mshikamano na askofu huyo katika
kuongoza na kuihubiri injili ya Yesu Kristo.
“Halmashauri kuu inaendelea kulifuatilia
jambo hili kwa makini. Washarika mnaombwa kuwa watulivu na kuliombea kanisa.
“Tunaombwa kutunza amani na umoja wa kanisa
kama neno la Mungu linavyosema,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Askofu Malasusa, Askofu wa Dayosisi ya
Kaskazini na Kati, Solomon Massangwa na Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki,
Dk. Lucas Mbedule, wanatuhumiwa kwa usaliti kutokana na uamuzi wao wa kuzuia
waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo usisomwe katika
dayosisi wanazoziongoza.
Jumapili iliyopita Askofu Mbedule alilazimika
kuomba radhi kutii maagizo ya Baraza la Maaskofu wa KKKT.
Waraka huo ulioandaliwa mwishoni mwa Machi
mwaka huu, wiki moja kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka, ulichambua
masuala ya jamii, uchumi, maisha ya siasa, umuhimu wa katiba mpya na matukio
yaliyo kinyume na kile walichokiita tunu na misingi ya taifa.
Licha ya barua hiyo ya kanisa kusomwa baadhi
ya waumini walihoji hatua hiyo kutokana na kutosomwa na waraka wa kanisa wa
Pasaka na badala yake wamesomewa barua ya kumkingia kifua Askofu Malasusa.
Hatua ya halmashauri kuu ya dayosisi hiyo
imeonyesha kumkingia kifua kutokana na barua iliyoandaliwa na chombo hicho na
ilisomwa jana.
Kwa mujibu wa nakala ya barua hiyo ,
Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo, imesema haikuwa na lengo la kupingana na
maazimio ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa KKKT juu ya kusomwa kwa
Waraka wa Pasaka.
Barua hiyo imesema maelekezo yote
yaliyotolewa yamezingatiwa na imesisitiza kuwa umoja na mshikamano kwa Askofu
Dk. Malasusa utaendelea katika kuongoza na kuihubiri Injili ya Yesu Kristo.
Barua hiyo ilieleza kuwa halmashauri hiyo
ilikaa kikao Mei 2, mwaka huu na ilijadili na kujiridhisha kuhusu barua
aliyoandikiwa Askofu Malasusa kuwa alikiuka mapatano yaliyotolewa na mkutano wa
maaskofu wa KKKT.
“Halmashauri Kuu imetafakari kwa kina jambo
hili na kujiridhisha kwamba: Haikuwa lengo la DMP kupingana na maazimio ya
Mkutano wa Maaskofu daima. Maelekezo yote yaliyotolewa na KKKT Makao Makuu
yamezingatiwa.
“Hata hivyo, Halmashauri Kuu imesikitishwa
kwa jinsi suala zima lilivyotunzwa hadi kufikia vyombo vya habari na baadhi yao
kupotosha ukweli wa suala zima,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Kuhusu Askofu Malasusa barua hiyo
ilisisitiza: “Washirika mfahamu kwamba Malasusa ni Askofu wa DMP. Halmashauri
inatoa pole nyingi kwa Baba Askofu na familia yake kwa usumbufu uliojitokeza.
DMP itaendelea na umoja na mshikamano na Askofu Malasusa katika kuongoza na
kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.”
Pamoja na barua hiyo kutoa pole kwa washirika
wote kutokana na kuumizwa kwao na taarifa za kuandikiwa barua Askofu Malasusa
za kukiuka mapatano ya Baraza la Maaskofu, ilizodai haikuwa lengo la KKKT Makao
Makuu kuwaumiza waumini wake, pia ilieleza inaendelea kulifuatilia jambo hilo
kwa makini.
Pia barua hiyo iliwaelekeza washirika hao
kuwa watulivu na kuliombea kanisa na kutunza amani na umoja.
Uamuzi wa kumtenga Askofu Malasusa ulifikiwa
na kikao cha Baraza la Maaskofu wapatao 25, lililoketi mjini Arusha, chini ya
kiongozi wake ambaye ndiye mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Fredrick Shoo.



