Mbunge John Mnyika Na Bulaya Watolewa Bungeni

Naibu Spika Tulia Ackson ameagiza
Mbunge wa Kibamba Mhe. John Mnyika na Ester Bulaya kutolewa nje ya ukumbi wa
Bunge kwa kile alichodai kutoheshimu kiti cha Spika.
Naibu Spika ametoa maamuzi hayo jioni
ya leo Mei 9, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji
mwaka 2018/19 ambapo Mbunge John Mnyika alisimama akitumia kanuni ya 69(1),
kutaka kuahirishwa kuhitimishwa kwa hoja ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ili
apewe nafasi ya kutoa hoja yake ya kwanini bajeti ya wizara hiyo isipitishwe na
Bunge.
Mara baada ya kauli hiyo, Dk Tulia
alisimama akitumia kanuni ya 69(2), kusema kama Spika atakuwa na maoni kwamba
kuwasilishwa kwa hoja hiyo ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge,
atakataa kuitoa ili ijadiliwe.
Hivyo kutokana na mabishano ya
kinanuni hayo yaliyojiri Naibu Spika Dk Tulia Ackson aliamuru Mnyika atolewe
nje kwa kutoheshimu kiti cha Spika.
Mbali na Mnyika Naibu Spika Dk. Tulia Ackson amemtoa pia ndani ya Ukumbi
wa Bunge, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) kwa kutoheshimu kiti
cha Spika.



