Rais MAGUFULI Awakubali Mabingwa Simba Sc

Shirikisho la soka
nchini TFF leo Mei 16, limethibitisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi na
kukabidhi vikombe vya ubingwa wa Serengeti Boys na Simba.
Mtendaji mkuu wa
TFF Wilfred Kidao amesema wamethibitishiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuwa Rais Magufuli amekubali kuwa
mgeni rasmi kwenye mchezo wa Simba SC dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi hii.
''Rais Magufuli
amekubali ombi la TFF kuwakabidhi vijana wa Serengeti Boys Kombe la CECAFA
waliloshinda hivi karibuni nchini Burundi, tukio ambalo litaambatana pia na
kuikabidhi Simba SC kombe la ubingwa wa VPL msimu huu'', amesema.
Serengeti Boys
wameibuka mabingwa wa soka katika ukanda wa Africa Mashariki na Kati baada ya
kutwaa ubingwa huo kwa kuwafunga vijana wa Somalia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo
wa fainali.
Simba imetwaa
ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2017/18 baada ya kufikisha
alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kati ya 16 za ligi kuu msimu
huu.



