TRA Yawataka Mawakili Kujisajili VAT,

Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Abdul Mapembe akizungumza na waandishi wa mara baada ya kufungua semina kwa mawakili na wanasheria jijini dar es salaam.
Na. Hussein Ndubikile
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imewataka Mawakili wote kujisajili kwenye mamlaka hiyo ili waingizwe katika makusanyo ya Kodi ya Ongezeko ya Mapato(VAT) huku ikibainisha itaanzisha oparesheni ya kuwakamata wananchi ambao hawadai risiti wanapofanya manunuzi ya bidhaa.
Aidha, mamlaka hiyo imewataka mawakili kuhakikisha wanawasilisha kodi hiyo kila mwezi lengo likiwa kuongeza makusanyo ya mapato.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Abdul Mapembe wakati wa Semina iliyoikutanisha mamlaka hiyo na mawakili ikilenga kuondoa sintofahamu ya masuala ya kodi baina pande zote mbili pamoja na kukumbushana wajibu wa kulipa kodi.
Amesema kuwa mawakili wengi wamekuwa hawana utamaduni wa kujisajili TRA ili kulipia VAT hali inayosababisha mapato kupotea hivyo anaamini semina hiyo ni chachu ya kuwapa uelewa mawakili umuhimu wa kulipa kodi.
“Sheria inawataka mawakili kujisajili katika Kodi ya Ongezeko ya Mapato pia wanatakiwa kuwasilisha mapato sahihi ya mwaka,” amesema.
Amebainisha kuwa semina hiyo ni endelevu na kwamba mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu kwa mawakili wa mikoa mingine ikiwemo Mbeya, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Amesisitiza kuwa katika semina hiyo mawakili wamewasilisha changamoto zao ikiwemo nyaraka za mikataba ya mauziano kutoaminiwa na TRA pamoja na za usajili.
Amefafanua kuwa wataanzisha oparesheni kabambe ya kuwakamata wale wote ambao hawadai risiti za bidhaa kwani vitendo hivyo vinaipotezea mapato mamlaka hiyo.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi ili wachukuliwe hatua stahiki.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa mamlaka hiyo, Abdul Zuberi amesema elimu iliyotolewa kwa mawakili hao itasaidia kuwafikishia wenzao ambao hawajajua umuhimu wa kujisajili kuingizwa kwenye VAT.
Naibu Kamishna Zuberi amewataka mawakili wawe mstari wa mbele wa kulipa kodi na kubainisha mambo yaliyojadiliwa yatafanyiwa kazi na mamlaka hiyo ili kuondoa changamoto zilizopo.
Naye Wakili, John Rugambo ameiomba TRA kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama ya mashine za Kielektroniki ili kuwavutia vijana na mawakili wanaotaka kuanza kufanya biashara.
Pia ameishauri mamlaka hiyo kuendesha mafunzo kwa watendaji wake kupunguza usumbufu wanaoupata wakati wakifutailia masuala mbalimbali.
Wakili Rugambo amependekeza mamlaka kutoa mashine za Efd bure na kuwalipisha kodi rafiki ya mapato ya mwaka



