Breaking News

BIL 1 KUJENGA VYUMBA VYA MADARASA 53 MISENYI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa, amesema Serikali kupitia fedha za Shirika la Fedha Duniani (IMF) tayari imetoa sh.bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 53 ya shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Pia, amesema Sh.milioni 200 zimetolewa kwa ajili ya kujenga Madarasa 10 ya shule shikizi.
Ameyasema hayo leo tarehe 18 Machi , 2022 wakati akitoa salamu katika Ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati wa Uzinduzi wa jengo ya kitega uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kilichopo Mutukula Misenyi Kagera.

Pamoja na hilo, Waziri Bashungwa amesema kwa Mwaka wa fedha wa 2021/22 Halmashauri hiyo yameshapokea sh.Milioni 695 kuendeleza sera ya elimu bila malipo katika shule za msingi na sekondari
Amesema kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekobdari (SEQUIP) Serikali imetoa sh. milioni 470 za ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata ambazo hazikuwa na shule za sekondari za kata.

Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa sh.milioni 262.5 zimetolewa kukamilisha vyumba vya madarasa vya shule za msingi na Sekondari ambapo madarasa 12 ya shule za sekondari na madarasa tisa ya shule za msingi sambamba na sh.milioni 150 za ujenzi wa maabara sita za sekondari.

Wakati huo huo, Waziri Bashungwa amelipongeza NHC kwa ujenzi wa jengo la kitega uchumi kitakachochea shughuli za biashara  katika eneo la Mtukula ambao ni mpaka wa Tanzania na Uganda.
Vile vile, ametoa wito kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angelina Mabula kupitia shirika hilo kukutana na kuweka mpango wa kujenga masoko na stendi za kisasa katika Halmashari na kuweka ubia wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI  kulipa kwa awamu.