LHRC, LEAT WAPENDEKEZA MAKAMU WA RAIS KUUNDA TUME HURU KUCHUNGUZA UCHAFUZI MTO MARA
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) wamemuaomba Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kuunda Tume huru itakayo wajumuisha Wanamazingira wanaoaminika na wenye weledi wa mkubwa wa kisayansi nchi kubani chanzo cha uchafuzi wa Mto Mara.
Akisoma mapendekezo hayo jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala alisema Makamu wa Rais anapaswa kuunda tume hiyo kwani yeye ndiye mwenye dhamana ya mazingira
Dkt. Nshala alitamka na kutaka mambo mengine ya kufanyiwa kazi kuwa ni kuhakikisha haki ya kuishi na kufanya kazi katika mazingira yaliyo safi na salama yanakuwa ni haki ya msingi na lazima iheshimiwe na wote ikiwemo watendaji wa Serikali na taasisi au kampuni binafsi.
Vile vile ametaka kukataliwa na kutupilliwa mbali kwa Ripoti ya Kamati ya Prof. Samuel Manyele kutokana na kuwa na upotoshaji mkubwa juu ya sababu za uchafuzi wa Mto Mara.
Kwamba kuwasilishwe mara moja kwa ripoti za usafishaji maji machafu zitolewazo kila mwezi na Kampuni ya North Mara Gold Mine ambayo mabwawa yake ya kuhifadhi maji machafu yako jirani na Mto Mara na eneo liliochafuliwa na kubaini ukweli wake na upotoshwaji wake.
Kupimwa kiwango cha uchafuzi katika eneo husika na kubaini kemikali na sumu zilizomo katika eneo hilo. Kuhojiwa kwa kina na bila vitisho wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na waathirika na kujua kiwango cha athari kwao binafsi na maeneo yao ya kufanyia kazi.
Mengine ni Serikali ichukue jukumu la kusafisha mara moja eneo lililochafuliwa na kudai fidia ya gharama hizo kutoka kwa mchafuzi kama itakiwavyo na kanuni ya "mchafuzi alipe". Kutolewa kwa fidia ya haki na ya haraka kwa waathirika wote wa uchafuzi huo.
“Wawajiboshwe watendaji wote wa Serikali waliohusika na ufichaji wa ukweli juu ya uchafuzi wa Mto Mara na wale walioshindwa kuchukua hatua za kupambana na uchafuzi wa uliotokea katika eneo hilo kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka huu,,”.
“Kuundwa upya kwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini kutokana na kushindwa kwake kuchukua hatua stahiki za kupambana na uchafuzi wa mazingira katika eneo la Mto Mara na nchini kwa ujumla. Kutengwa kwa bajeti kubwa ya kutoa elimu na miundomfumo ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira nchini na hatua madhubuti zichukuliwe na Serikali kuwanusuru wakazi, mifugo na mazingira ya Mto Mara na Ziwa Victoria kwa ujumla kutokana na uwepo wa athari zinazoendelea,” amesema.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Anna Henga amesema amebainishwa kwamba mnamo Machi 8, 2022 iliripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini uwepo wa uchafuzi wa mazingira uliosababisha uchafuzi wa maji ya mto Mara na kuonekana kwa samaki waliokufa wakielea kwenye Mto Mara kutokana na uchafuzi huo.
“Kutokana na taarifa hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) vimefuatilia ili kuweza kujiridhisha juu ya taarifa hizo na kuona jinsi gani wahanga wa haki za mazingira na haki za binadamu wanaweza kusaidiwa endapo haki hizo zitakuwa zimekiukwa,”.
“Kwa minajili hiyo, LHRC na LEAT vilifuatilia na kutembelea baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimeonekana kuathirika ili kubaini chanzo na athari zilizosababishwa na uchafuzi huo. Na kuanzia tarehe 17 hadi 20 Machi 2022 vilitembelea maeneo yanayozunguka na kutegemea huduma na matumizi ya maji kutoka Mto Mara”.
Amesema maeneo yaliyotembelewa na kufanyiwa uchunguzi ni vijiji vya Kirumi na Bisarwi vilivyoripotiwa kuathirika zaidi. Aidha, ameeleza, Timu ya uchunguzi ya taasisi hizi mbili ilifanya mahojiano na wananchi wa vitongoji mbalimbali ikiwemo vitongoji vya Makora, Burongo, Bisarwi kati na Kwikoma vilivyopo kata ya Manga Wilaya ya Tarime mkoani Mara na kubaini kuwepo kwa taarifa za vifo vya mifugo na wakazi wa maeneo hayo vinavyotokana na kunywa maji ya Bonde la Mto Mara.
Amesema kwa upande mwingine LHRC na LEAT vimefuatilia kwa ukaribu taarifa zilizotolewa na Kamati Maalumu ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jaffo kwa lengo la kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji ya Mto Mara na kubaini kuwepo kwa upotoshaji.




