LHRC YALAANI JARIBIO LA KUTAKA KUKATWA MKONO MTU MWENYE UALBINO DAR
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani Jaribio la kutaka kukatwa mikono kwa mtu mwenye Ualbino Mohamed Rajabu mkazi wa Kata ya Mabibo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za tukio hilo.
Alisema kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa katika Kituo cha Runinga cha Azam TV na mitandao ya kijamii kwamba Mohamed Rajabu alishambuliwa Aprili 25 mwaka huu na watu wasiojulikana waliokuwa na lengo la kumkata mikono yake.
“Baada ya kiripotiwa taarifa hii na kituo kimoja cha television na badae kusambaza katika mitandao ya kijamii Kituo kimechukua hatua za haraka kuanza kufanya utafiti ili kubaini ukweli juu ya taarifa hii ya kusikitisha ambapo tumebaini taarifa ni za kweli licha ya kutothibitishwa na Jeshi la Polisi mpaka sasa,” Alisema wakili Henga.
Alisema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wakiwemo wanafamilia wahalifu hao walijaribu kutaka kumkata mikono kitendo ambacho hakikufanikiwa hivyo kumjeruhi kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Wakili Henga aliongeza kuwa katika kipindi cha takribani miaka mitano, kuanzia 2015 hadi 2020 hakukuwa na ripoti ya matukio yoyote ya mauaji dhidi ya watu wenye Ualbino nchini.
Amesema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na juhudi za pamoja kati ya Jeshi la Polisi Tanzania, Mahakama, Asasi za kiraia na Tume ya Haki za Binadamu nchini kufanya juhudi kubwa katika kukemea, kuwakamata wahusika na kuwapa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria
“Wasiwasi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni kurudi kea soko haramu (Black Market) la viungo vya watu wenye Ualbino, soko ambalo lilidhibitiwa kwa zaidi ya miaka mitano,” Alisema Wakili Henga.
Napenda kuchukua nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa tukio hii wanakamatwa, upelelezi inafanyikia kwa wakati na kufikishwa Mahakamani na kupatiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.




