WAGOMBEA TLS WAJINADI, DK. HOSEA AELEZA ALIYOFANYA AKIOMBA KUCHAGULIWA TENA
WAGOMBEA Urais wa Chama cha Wanasheria wa Tangayika (TLS), wameeleza vipaumbele vyao watakavyofanya wakichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa cham hicho unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mei, 2022.
Wagombea hao ambao ni, Harold Sungusia, Profesa Edward Hosea na Jeremiah Mtobesya, wametaja vipaumbele hivyo jana Jumatano, katika mdahalo wa wagombea urais ulioandaliwa na TLS na kuongozwa na Jenerali Ulimwengu.
Akizungumza katika mdahalo huo Sungusia, alisema amejitosa katika kinyang’anyiro hicho, baada ya kuona chama hicho kimeshindwa kupeleka maoni yake bungeni kuhusu miswada ya sheria mbalimbali.
Sungusia alisema, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa TLS, atarudisha mchango wa chama hicho katika masuala yanayogusa maslahi ya nchi.
“Nataka kurudisha ile relevance ya TLS, mara nyingine watu wanauliza TLS iko wapi? wakili amekamtwa TLS iko wapi? Ninahitaji kuona TLS ambayo ni relevance na inapokuja ajenda ya kitaifa mfano katiba, lazima relevance ya TLS iweze kuonekana,”alisema Sungusia.
Naye Mtobesya, aliahidi kuimarisha uhuru wa chama hicho pamoja na kuongez a mapato yake, endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo.
“Suala lingine nitakalofanyia kazi ni independence of the bar (uhuru wa chama). Mawakili wenzetu mara nyingi tumewaona wakiingiliwa wakati wanafanya kazi zao, wakati mwingine anakuw akatika mgogoro na sheria bila sababu. Iwapo nitapata wasaa tutahakikisha tunawasaidia wakiwa kwenye mgogoro,” amesema Mtobesya.
Mtobesya amesema “tutatetea haki zao katika mfumo wa kistaarabu kwa kufuata sheria, sababu sheria zipo. Tutahakikisha haki ya wakili inapatikana bila kugandamiza haki yake.”
Aidha, ameahidi endapo atachaguliwa kuwa Rais wa TLS, atahakikisha chama hicho kinatekeleza majukumu yake katika kusimamia Bunge na Mahakama, kwa kutumia mpango kazi wake.
Kwa upande wake Prof. Hoseah, amesema ataendelea kutumia dhana yake ya maridhiano kuimarisha mahusiano ya TLS na mihimili ya nchi, Bunge, Mahakama na Serikali.
“Nimetumia dhana yangu kuhakikisha Serikali , Bunge na Mahakama tunashirikiana na kuondoa dhana potofu kwamba hatuwezi kushirikiana na Serikali, nyie mmeona wakati wangu TLS imetulia na kufanya kazi kitaaluma,” amesema Prof. Hosea.
Akitaja mafanikio ya uongozi wake, Prof. Hoseah alisema, Serikali imekubali kutenga Sh. 1.4 bilioni, kwa ajili ya ruzuku kwa TLS katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.
“Nimeshaongea na Serikali nasubiri bajeti ambayo inaanza mwezi wa June, Wizara ya Katiba na Sheria imekubali kutenga Sh. 1.4 bilioni kwa ajili ya ruzuku katika zoezi la kusaidia misaada ya wananchi. Sababu TLS inatekeleza jukumu la umma,” alisema Dk. Hoseah.
Prof. Hoseah amesema, amefanikiwa kuishawishi Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa Kituo cha Usuluhishi cha Kimataifa Tanzania, ambapo imekubali kutoa kiasi cha Sh. 1.2 bilioni.
Pia, Prof. Hoseah amesema katika kipindi cha uongozi wake amefanikiwa kuishawishi Mahakama Kuu ya Tanzania, kurejesha tozo za ada zinazotolewa na mawakili kiasicha Sh. 450, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati akigombea nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa mwaka jana.




