TALGWU YATOA UFAFANUZI KUFATIA KUWEPO UPOSHWAJI JUU YA UPIGWAJI FEDHA ZA CHAMA
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Bwana Rashid Mtima akifafanua jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliyofanyika 26 Mei jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam:
OFISI ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) imekanusha habari zilizotolewa na Gazeti la Jamuhuri kuhusu kupigwa kwa fedha za chama kwenye zabuni ya kutengeneza sere za Mei Mosi, 2022 na utata wa manunuzi ya gari.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa TALGWU Taifa Bw. Rashid Mtima amesema habari hizo ni zaupotoshaji zenye lengo la kuvuruga mshikamano uliopo na kuleta chuki kati ya wanachama na uongozi.
Mtima ameeleza kwamba Mei 10-16 mwaka huu gazeti hilo lilisomeka kuwa “Fedha za TALGWU zapigwa”, kwamba kwa nia ovu mwandishi wa habari husika alikuwa na lengo la kuichafua TALGWU na kuzua taharuki kwa wanachama wake na wadau wengine ambao wanashirikiana na TALGWU kwa namna moja ama nyingine.
“Naomba ieleweke kwamba mchakato wa manunuzi ya sare za Mei Mosi za mwaka 2022 ulizingatia taratibu zote za manunuzi kwa mujibu wa kanuni za manunuzi ya Chama za mwaka 2018 na kitabu cha zabuni namba TALG/PROC/0021/2021 na kupelekea kumpata mzabuni Savana General Merchandise ambaye alipewa kazi ya uchapaji na usambazaji wa sare 80,000 zenye thamani ya 1,196,000,000,” Alisema Bwana Mtima.
Alisema baada ya mapokezi ya sare hizo ikagundulika kwamba kuna mapungufu makubwa ya ubora wa sare ikilinganishwa na makubaliano kwa mujibu wa mkataba, ndipo ofisi ilipochukua maamuzi ya kumjulisha mzabuni kuhusu mapungufu hayo na kumtaka kusimamisha zoezi la usambazaji sambamba na kuwajulisha makatibu wa mikoa ambayo ilishapokea kutozigawa kwa wanachama kwa sababu ya mapungufu makubwa yaliyogundulika.
Amebainisha kuwa taratibu za ndani kwa kuzingatia kitabu cha zabuni, kanuni za manunuzi ya chama toleo la mwaka 2018 na mkataba zinaendelea.
“Baada ya ufafanuzi huo nilioutoa wa mchakato mzima wa sare za Mei Mosi, 2022 hadi hatua tuliyofikia mpaka sasa, napenda kutoa taarifa kwa umma kwamba gazeti la Jamhuri limepotosha ukweli halisi wa manunuzi ya sare za Mei Mosi za TALGWU ,” amesisitiza Mtima.
Akifafanua kuhusu fedha za TALGWU kiasi cha shilingi bilioni 1.1 za kuchapa sare 80,000 kupigwa, Mtima ameeleza kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani mpaka sasa Mzabuni Savana General Merchandise amelipwa jumla ya shilingi 700,000,000.00 kwa mujibu wa mkataba na sio shilingi bilioni 1.1 kama ilivyoripotiwa.
Kuhusu sare za Mei Mosi, 2020 amesema ununusi wa sare hizo uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.1 na sio shilingi bilioni 1.2 kama ilivyoripotiwa na mwandishi wa gazeti hilo.
“Idadi ya sare zilizochapishwa kwa ajili ya Mei Mosi ya mwaka 2022 zilikuwa fulana 90,000 na kofia 90,000 kulingana na kitabu cha zabuni namba TALG/PROC/0020/2020 na mkataba wa uchapishaji wa sare hizo na hakukuwa na utata wowote katika mkataba kama ilivyoelezwa kwenye gazeti hilo,” ameongeza Mtima.
Akizungumzia kuhusu sare za Mei Mosi za mwaka 2019, Mtima ameeleza kuwa gazeti hilo liliripoti kwamba katika zabuni ya sare za Mei Mosi mwaka 2029 kulikuwa na udanganyifu kwa kutengeneza sare 60,000 lakini malipo yaliyofanywa ni sare 80,000 na kofia hazikupelekwa jambo lililolazimu mikoa kununua kofia za wanachama.
Katibu Mkuu amebainisha kuwa huo ni upotoshaji na uongo uliokithiri wenye dhamira ovu ya kuichafua TALGWU na uongozi wake kwani ukweli ni kwamba ununuzi wa sare hizo uligharimu shilingi milioni 934,560,000 kwa idadi ya fulana 80,000 na kofia 80,000 na haijawahi kutokea ofisi za mikoa kukosa kofia na kujinunulia zenyewe.
Akizungumzia teleo la Mei 24-30, 2022 lililosomeka “Utata ununuzi magari ya TALGWU”, amesema kwamba gazeti hilo limekuwa na lengo la kuendelea kuichafua TALGWU na kuzua taharuki kwa wanachama wake bila sababu za msingi. Hivyo ameeleza kuwa taarifa iliyoandikwa kuhusu utata katika ununuzi wa magari ya TALGWU imepotosha umma.
“Madai ya Gazeti la Jamhuri kwamba fedha za ununuzi wa gari ya Katibu Mkuu zilitosha kununua jipya lakini likanunuliwa la mtumba. Napenda ieleweke kwamba, machakato wa ununuzi wa gari hili ulizingatia taratibu zote za kanuni za manunuzi ya chama toleo la mwaka 2018, bajeti ya Chama na hali ya kifedha,” amsema Mtima.
Aidha kuhusu fedha zilizonunua gari hiyo kutosha kununua gari jipya, ametaka ieleweka kuwa TALGWU haikuwahi kudhamiria kununua gari jipya kwa kuwa uwezo wa kutenga milioni 400 kwa ajili ya gari la Katibu Mkuu hawana.
Alisema chama kilitenga fedha za kununua gari ya mtumba aina ya Toyota Land Cruiser V8.
Amesema kuwa kutokana na taarifa hiyo kuleta mkanganyiko mkubwa kwa viongozi na wanachama hali iliyoweza kupelekea kukosa imani na Chama chao ambacho kimekuwa kikifanya juhudi kubwa za katika kutetea haki na maslahi yao wakiwa kizani.
TALGWU imejipanga kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya gazeti hilo kwa kutoa taarifa zenye lengo la kuchafua taswira ya chama na kukidhalilisha




