Breaking News

LHRC YAWALETA PAMOJA WADAU KUTATHMINI MIAKA 30 YA DEMOKRASIA NCHINI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeadhimisha siku ya Demokrasia Duniani kwa kufanya kongamano kubwa lililowakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali kutathmini miaka 30 ya Demokrasia tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Bi Felista Mauya amesema lengo kubwa la LHRC kuandaa kongamano hilo ni kutokana na kuwa mdau na mtetezi mkubwa wa haki za binadamu.

“Leo tunadhimisha hapa kuadhimisha siku hii muhimu kwa lengo la kuendeleza na kuunga mkono jitihada za kukuza na kulinda haki za binadamu,” Alisema Felista.

Alisema Demokrasia ni kielelezo tosha cha ustawi wa haki za binadamu, pia ni ishara ya kuendeleza utamaduni wa ustaarabu na utii wa Sheria hivyo uwepo wa Demokrasia ni kiashiria cha utekelezaji wa dhana ya ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika kufanya maamuzi ya kuchaguaviongozi wao.

Kwa upande wao wadau na washiriki wa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba amesema hali ya Demokrasia nchini imekuwa ikisuasua katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

“Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuandika Katiba Mpya na kufanya mabadiliko ya Sheria 40. Kuliendelea mbele bila kuwa na msingi mzuri wa kikatiba na sheria,” ameeleza Prof. Lipumba.

Mbunge wa Ubungo (CCM) Prof. Kitila Mkumbo amesema, ili wananchi washiriki vizuri katika Demokrasia ni lazima miiba iondolewe.

“Ni vizuri iandikwe Katiba ambayo itaongeza ushiriki wa wananchi katika Demokrasia. Katiba ikiendelea namna hii, mtaendelea kulia kila mwaka,” amesema Prof. Mkumbo.

Naibu Katibu Mkuu Bara wa ACT-Wazalendo Joram Bashange amesema “Tunahitaji kuwekeza kwa wananchi kwenye elimu ya Uraia,”. 

Alisema kuwa kama ACT-Wazalendo wametoa mapendekezo yao kwenye kikosi kazi kwamba ubadilishwe mfumo wa uchaguzi.

“Tutoke kwenye first past the post, twende kwenye proportional representation. Hii itaongeza ushiriki wa wananchi katika Demokrasia,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Neema Rugangira amesema kuwa ni vizuri kukawa na utaratibu wa kutenga nafasi Fulani za majimbo kwa ajili ya wanawake kwamba hiyo itavifanya vyama kuwajengea uwezo wanawake. 

Wadau mbalimbali walioshiriki katika mjadala wa maadhimisho ya siku ya Demokrasia duniani ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).