Breaking News

SERIKALI YAOMBWA KUCHANGIA MFUKO WA GLOBAL FUND

Mkurugenzi Mtendaji wa Health Promotion Tanzania (HDT) Dkt. Peter Bujari akifafanua kuhusu ushiriki wa serikali katika uchangiaji wa Mfuko wa Kimataifa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .

Dar es salaam
HEALTH Promotion Tanzania (HDT) imeiomba serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuangalua namba ambavyo inaweza kuchangia mfuko wa Global Fund kama nchi nyingine.


Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa (HDT), Dkt. Peter Bujari amesema tunaiomba serikali kuangalia namna ambavyo itaweza kuanza kuchangia mfuko huo wa kimataifa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malalia.

“Tunaomba nchi yetu ionyeshe ushirikiano na nchini zingine katika kuchangia mfuko huu. Hivyo Serikali yetu ni sikivu tunaomba iahidi kuchangia katika mfuko na tusiwe wa kupokea tu,” amesema Dkt. Bujari na kuongeza kwamba,

“Mafanikio ya Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ni mafanikio na maendeleo ya wananchi wa Tanzania, hasa wale wa kipato cha chini,”.

Dkt. Bujari amebainisha kwamba kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikishirikiana na na Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na Maradhi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) katika kupanga na kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na maradhi hayo.

Amesema Global Fund ni moja ya wafadhili wakubwa duniani na nchi ya Tanzania katika kufikia malengo ya sasa ya kutokomeza maambukizi mapya ya kifua kikuu na virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

“Michango ya Global Fund imesaidia kupunguza maambukizi mapya, kuwapatia matibabu wagonjwa na hivyo kupunguza vifo na kuwawezesha wengi kushiriki shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Hata hivyo ugonjwa wa Kifua Kikuu umeendelea kuwa tishio kubwa nchini na duniani ambapo, kwa mara ya kwanza, katika muongo mmoja uliopita, idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kifua kikuu imeongezeka kwa mwaka 2020. Hali hii haikubaliki,” Alisema Dkt. Bujari.

Dkt. Bujari ameendeelea kueleza kuwa ili kufikia malengo ya kutokomeza maradhi ya Kifua Kikuu na UKIMWI, kwa miaka mitatu ijayo, zinahitajika Dola za kimarekani bilioni 130.2 na Global Fund pekee yake inahitaji dola za kimarekani bilioni 18.

Kwamba fedha hizo zitachangia kuendeleza mapambano ya kutokomeza maradhi hayo kwa kujenga ustahamilivu na mifumo ya endelevu ya afya na kuimarisha utayari katika kukabiliana na maradhi, hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania ambapo hiyo itasaidia kufikia watu milioni 20 ifikapo mwaka 2026.

Amesema katika Sekta ya Afya kwa Tanzania pekee, mfuko huo umeweza kuchangia kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.6 toka mwaka 2002 ambapo fedha hizo zimesaidia kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Kwamba zaidi ya watu milioni 1.2 waliweza kufikiwa na kupata huduma za dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi, zaidi ya watu milioni 8.2 wamepata huduma na kupona Malaria, neti milioni 4 zimegawiwa bure nchi nzima, zaidi ya watu elfu 84 wamepona Kifua Kikuu na zaidi ya watu 391 wenye Kifua Kikuu sugu wapo kwenye matibabu.

Amebeinisha kuwa kidunia Mkutano Mkuu wa uchangiaji wa Mfuko kwa Awamu ya saba utafanyika nchini Marekani kuanzia Septemba 19 hadi 21 mwaka huu kwamba fedha hizo zinategemewa kuokoa maisha ya wanadamu zaidi ya milioni 20 duniani kote ifikapo mwaka 2026.