BRELA YAKUTANA NA WADAU KUHUSU MABADILIKO YA SHERIA YA LESENI ZA BIASHARA
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)
umekutana na wadau ili kupata maoni na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya
Leseni za Biashara Sura 208 ya mwaka 1972.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 14, 2022
jijini Dar es Salaam wakati wa kikako hicho Mkurugenzi wa Leseni kutoka BRELA
Andrew Mkapa amesema maoni hayo yatafanyika kwa siku tatu.
Amesema leo wameanza kwa kukutana na wadau kutoka
taasisi mbalimbali za Serikali, kesho watakutana na watu wa Sekta Binafsi huku
kesho kutwa ikiwa ni siku ya majumuisho ya maoni hayo kwa ajili ya kupelekwa
kwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa hatua nyingine.
“Nadhani wote mnafahamu kuna suala la leseni ya
biashara ambapo wafanyabiashara wanapofanya biashara ni lazima wawe na leseni
za biashara. Utoaji wa leseni ya Biashara unasimamiwa na Sheria ya Leseni ya
Biashara sura 208,” amesema Mkapa na kuongeza,
“Kwahiyo BRELA ikiwa kama moja wapo ya mamlaka inayotoa
hiyo leseni ya biashara, ilifanya mchakato wa kuwasiliana na Wizara Mama Wizara
ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ambayo Waziri wake ndiyo mwenya dhamana mama
ya kusimamia Sheria hii, kwa ajili ya kufanya mabadiliko mbalimbali kwenye
Sheria hii ili kuendana na wakati na mabadiliko yanayotokea,”.
Hivyo amesema kuwa sheria hiyo kama ilivyosheria kwa
Sheria nyingine za nchi haitakiwi kuwa mgando inatakiwa kwenda na mabadiliko ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayoendelea duniani na hapa nchini.
“Katika kufanya utekelezaji wa mabadidiko hayo, Wizara
ya Viwanda na uwekezaji iliunda kikosi kazi ambacho kilikaa na kukusanya
mapendekezo ya awali kwa ajili ya marekebisho ya sheria hii na baada ya
kuwasilisha mapendekezo hayo Waziri Mwenye dhamana na Masuala ya Biashara
aliagiza kwamba anataka kupata maoni ya wadau ambao kwa namna moja ama nyingine
wanaitumia hii sheria,”.
Mkapa amebainisha kwamba Kikako ambacho BRELA
imekiandaa ni agizo la Waziri wa Uwekezaji na Viwanda na Biashara ili kuweza
kupata maoni ya wadau ili kupata mapendekezo kwa ajili ya maboresho ya Sheria
hiyo.




