Breaking News

DKT. CHANG’A ATOA WITO KWA VIJANA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA SAYANSI NA TATHMINI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI

UNFCCC COP28, Dubai, UAE
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi “Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC)”, Dkt. Ladislaus Chang’a, ametoa wito wa kuimarisha ushiriki wa vijana katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC).

Dkt. Chang’a alitoa wito huo tarehe 8 Desemba, 2023 kwenye Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi “United Nations Climate Change Convention Conference of Parties (UNFCCC COP28) ”, uliofanyia Jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba, 2023. 

Alitoa wito huo alipoongoza mjadala kuhusiana na “Mabadiliko katika Mfumo wa elimu kuwajengea uwezo vijana, na Uimarishaji wa ushiriki wa vijana katika sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na shughuli za Jopo la IPCC (Transforming education to empower youth and enhancing the participation of young people in climate change science and IPCC process: challenges, opportunities, lessons learned) ”. Mjadala huo uliandaliwa na jopo la IPCC kwa kushirikiana na kampuni za “Philanthropy Cortes Solari” na “MERI Foundation”.

Akifungua mjadala huo, Dkt. Chang’a alitaja na kufafanua vipaumbele vya IPCC katika Mzunguko wa Saba wa Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi “Seventh IPCC Assessment Cycle (AR7). Kipaumbele kimojawapo alichoainisha ni kuimarisha ushiriki wa vijana katika mchakato mzima wa Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Duniani.

“Kipaumbele hiki cha IPCC kinalenga kuimarisha ushiriki wa vijana, sio tu katika upatikanaji wa taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, bali katika mchakato mzima wa tathmini yenyewe na ikiwa ni pamoja usambazaji wa taarifa ya tathmini”. Alisema Dkt. Chang’a. 

Aidha alifafanua kuwa mjadala huo ulijielekeza zaidi kujadili changamoto, fursa, mambo ya kujifunza na faida zinazotokana na ushiriki wa vijana katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shghuli za IPCC, kwa lengo la kukuza ushiriki wa vijana katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC, hususan wakati wa Tathmini ya Saba ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.

Mjadala huo ulihusisha mada mbalimbali zilizohusiana na lengo la mjadala huo. Miongoni mwa waliowasilisha mada ni baadhi ya viongozi wa Jopo la IPCC wa sasa na waliomaliza muda wao, mwakilishi kutoka Sekretarieti ya IPCC, maafisa viungo wa nchi katika Jopo la IPCC (IPCC Focal Points), na wawakilishi kutoka mashirika yanayojihusisha na vijana na watoto, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto la UNICEF.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na: Fursa zinazotolewa na IPCC kwa vijana ikiwa ni pamoja na Programu ya Ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya utafiti kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na faida za ufadhili huu. Aidha watoa mada wengine walijikita katika kuainisha changamoto za ushiriki mdogo wa vijana na mikakati ya kukabiliana na hizo changamoto ili kuimarisha ushiriki wa vijana.

Hii ilijumuisha watoa mada walioainisha uzoefu kutoka Mabara ya Afrika na Ulaya na nchi mbalimbali kama vile Japan, Ghana na Kenya. Aidha, washiriki wa mjadala huo walitoa michango na ushuhuda wa namna wanavyohusisha vijana katika masuala ya kukabiliana namabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalitolewa ufafanuzi.

Akihitimisha mjadala huo, Dkt. Chang’a alisisitiza kwamba licha ya changamoto zilizotolewa, uimarishaji wa ushiriki wa vijana katika masuala ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC, inawezekana na ni muhimu kuhakikisha vijana wanachangia ipasavyo katika kutatua changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Duniani.

“Uimarishaji wa ushiriki wa vijana katika masuala ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC ni muhimu sana na tumejipanga kufanya hivyo katika miaka saba ijayo”. Alisema Dkt. Chang’a na kuwahakikishia washiriki kuwa mawazo yote yaliyotolewa yatazingatiwa na IPCC katika kufanya maboresho stahiki. Pia aliwashukuru washiriki kwa michango mbalimbali waliyotoa katika mjadala huo.

Sanjari na mjadala huo, Dkt. Chang’a alishiriki pia katika vikao mbalimbali vilivyohusu mchango wa vijana na watoto katika mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ambapo aliendelea kuwasisitiza vijana na watoto kuwa chachu ya mabadiliko kwa kushiriki katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC. “Vijana na watoto ni mawakala wazuri sana wa mabadiliko na kwa hivyo wana jukumu muhimu sana katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi”, Alisema Dkt. Chang’a. 

Miongoni mwa vikao alivyoshiriki ni Mdahalo wa Vijana na Watoto kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (Youth and Children Climate Change Dialogue) ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF tarehe 8 Desemba, 2023 kujadili athari za mabadliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa watoto na vijana.

Aidha, Dr. Chang’a alikutana na Umoja wa Mtandao wa Taasisi za vijana (YOUNGO) unaojishughulisha na kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuwahamasisha kushiriki ipasavyo katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC. 

Dkt. Chang’a pia alikutana na vijana na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Japan, Norway, Eswatini, Equador, Mexico, Tonga and Tuvalu kwa lengo hilohilo la kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za IPCC.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alialikwa kuwa miongoni mwa wazungumzaji (Panelist) katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuhusiana na faida za huduma za hali ya hewa katika shughuli za kiuchumi (Socio-economic benefits of weather and climate services) uliofanyika tarehe 8 Desemba, 2023. 

Vilevile alishiriki katika mkutano ulioandaliwa na viongozi wa IPCC uliohusu uwasilishaji wa taarifa ya Tathmini ya Sita ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi na kuainisha mapungufu ya kushughulikiwa katika tathmini ya saba. Aidha, Dkt. Chang’a alifanya kikao na Ujumbe wa Wizara ya Elimu, Utamaduni, Michezo, Sayansi na Teknolojia ya Japan na kujadili masuala ya ushirikiano katika kujenga uwezo wa wataalamu katika masuala ya hali ya hewa na mchango katika mfuko wa ufadhili wa wataalamu wa IPCC.

Ikumbukwe kwamba Mkutano wa COP28 hufanyika sambamba na mikutano ya pembezoni (side events) na mikutano ya uwili (bilateral meetings). Katika mkutano wa COP 28, Dkt. Chang’a akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA alikuwa sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ambapo ushiriki wa TMA katika mkutano huo ulikuwa fursa ya kutoa mchango wa kitaalam kuhusu sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa katika majadiliano na maamuzi ya COP28 kwa manufaa mapana ya nchi yetu. 

Aidha, Dkt. Chang’a akiwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la IPCC, alishiriki katika programu na vikao vilivyoandaliwa na WMO na IPCC sambamba na mkutano huo wa COP28. 

Pamoja na majukumu mengine katika uongozi wa jopo la IPCC, Dkt.Chang’a amepewa na IPCC jukumu maalumu la kuratibu na kuhamasisha vijana duniani kote kushiriki na kutoa mchango katika Sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo na kushiriki katika shughuli za IPCC, jukumu ambalo alilitekeleza kwa ufanisi wakati wa Mkutano wa COP28.