MH. MAJALIWA: FANYENI MAZOEZI KUEPUKA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) wameshiriki katika uzinduzi wa mazoezi ya kila Jumamosi ambayo yameshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo taasisi zilizo chini ya wizara ya afya.
Akizindua mazoezi hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kushiriki mazoezi hayo kwakuwa yanajenga afya na yanasaidia kuepusha magonjwa yasiyoambukiza.
“Kipindi cha nyuma magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la damu tulikuwa tunadhani ni magonjwa ya matajiri lakini siku hizi yanawaathiri watu wote, ikiwemo vijana na wazee hivyo inatupasa watu wote kuchukua hatua kukabiliana na magonjwa haya” ameongeza Mh. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu amesema kwa siku za hivi karibuni magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la damu yamekuwa miongoni mwa magonjwa kumi yanayoongoza kuathiri Watanzania.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi amesema hospitali imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwashauri watumishi wake kuepuka tabia bwete kwa kufanya mazoezi na kuzingatia ushauri wa wataalam wa lishe.
Mazoezi ya kila Jumamosi yaliyozinduliwa leo yatafanyika kupitia Barabara iliyopo pembezoni mwa fukwe, kuanzia eneo la Coco beach kupitia Daraja la Tanzanite hadi makutano ya Barabara ya Aghakan na kuelekea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.





