WAZIRI JAFO AITAKA TIRDO KUKAMILISHA MFUMO WA UTAMBUZI WA FURSA ZA VIWANDA NCHINI
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Said Jafo ametoa agizo kwa shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kukamilika kwa mfumo wa ukusanyaji na utambuzi wa fursa za Viwanda nchini.
Akizungumza mapema leo Julai 22, 2024 ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa katika Wizara hiyo tarehe 2 Julai 2024 amesema kukamilika kwa mfumo huo unaoratibiwa na TIRDO chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika mwaka huu wa fedha kabla ya kufika Juni 2025 utasaidia upatikanaji wa taarifa hivyo kuleta manufaa kwa sekta ya Viwanda na taifa kwa ujumla.
"Nitoe wito kwa shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kukamilika kwa mfumo wa ukusanyaji na utambuzi wa fursa za Viwanda katika mwaka huu wa fedha, fanyeni mtakavyofanya lakini ifikapo Juni 2025 huu mradi uwe umekamilika". Alisema Jafo
Mapema akitoa taarifa ya Shirika, kaimu Mkurugenzi wa TIRDO Mha. Ramson Mwilangali alisema shirika limekuwa likiendelea kufanya tafiti mbali mbali katika sekta ya Viwanda nchini ili kuibua fursa nchini.
Amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na Kukamilisha Mfumo wa kanzidata ya taarifa za viwanda nchini (National Industrial Information Management System – (NIIMS), Kufanya Tathmini ya Viwanda katika Kanda ya Ziwa na Kuainisha Fursa za Uwekezaji, Kuanzisha Maabara ya Nishati na Madini Mkoa wa Njombe na Ludewa na Kutoa Elimu ya Utengenezaji na Matumizi ya Nishati Mbadala (Safi)
Bw. Mwilangali amezitaja nyingine kwa ni Miradi wa Kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Utawala ili Kutoa Nafasi ya Kuanza Kituo cha Taarifa za Viwanda (NIIMS) na Ubashiri wa Teknolojia na Viatamizi kwa Wabunifu wa Teknolojia Katika Shirika Pamoja na Kubadili ithibati ya maabara ya microbiology ya chakula kutoka bodi SANAS kwenda Bodi ya ithibati ya SADCAS.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TIRDO, Mhe Bashiri Juma Mrindoko alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kumhakikishia kuwa bodi yake itashirikiana na menejiment kwa ukaribu ili kufikia malengo ya shirika na kusimamia maagizo yote ya Serikali.
Ziara hiyo ya siku moja Waziri Jafo aliambata watumishi wengine wa Wizara wakiingozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhe Balozi Dkt .John Stephen Simbachawene ambaye alimhakikishia Mhe.Waziri kuwa maagizo yake yatatekelezwa na kufanyiwa kazi kwa wakati.








