Breaking News

KAFULILA: USHIRIKIANO WA PPP MUHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA

Dar es Salaam — Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema kuwa dhana ya Public-Private Partnership (PPP) ni muhimu kwa ustawi wa taifa, kwa kuwa inalenga kuisaidia Serikali kukuza uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kongamano la kitaifa kuhusu ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, Kafulila aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya PPP katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kafulila alisema ushirikiano kati ya sekta hizo unatoa fursa kwa sekta binafsi kusaidia Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hususan ile inayohitaji rasilimali kubwa na haimo katika bajeti ya kawaida ya Serikali.

"PPP si tu inasaidia kuvuta teknolojia mpya, bali pia inaleta ufanisi wa kiutendaji kwa sababu sekta binafsi ina uzoefu mkubwa wa menejimenti," alisema Kafulila.

Aidha, alieleza kuwa kupitia ushirikiano huo, Serikali inapunguza mzigo wa kifedha na kiutendaji, huku ikihakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

"Sekta binafsi ni mshirika muhimu katika kuhakikisha Serikali inamudu mahitaji ya wananchi wake kwa wakati," alisisitiza Kafulila.

Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kuimarisha ushirikiano baina yao kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa.