DKT. JEJE: HALMASHAURI ZIHAMASISHE PPP ILI KUIMARISHA MAENDELEO BILA KUTEGEMEA SERIKALI KUU
Dar es salaam - Mhadhiri Mwandamizi kutoka Taasisi ya Uhasibu Arusha, Dkt. Kafigi Jeje ametoa wito kwa watendaji wa halmashauri zote nchini kuchukua hatua thabiti katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Akiwasilisha mada kuhusu 'Nafasi ya PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa' wakati wa kongamano la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) mkoani Dar es Salaam, Dkt. Jeje amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 wananchi hawawezi kutegemea Serikali Kuu pekee, bali PPP ni daraja la kweli la maendeleo.
Ameeleza kuwa wakati Serikali inalenga kutoa huduma kwa wananchi wote, sekta binafsi ina nafasi ya kusaidia jitihada hizo kwa njia ya uwekezaji wenye tija na faida.
Dkt. Jeje amesisitiza umuhimu wa halmashauri kuwa na ubunifu, kujitegemea, na kutumia PPP kama nyenzo ya kuimarisha huduma, kuongeza ufanisi na kukuza maendeleo ya miji na vijiji bila kusubiri fedha kutoka juu.




