CHINI YA RAIS SAMIA SERIKALI YAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA BANDARI YA BAGAMOYO YENYE GHARAMA YA TRILIONI 26
Serikali ya Tanzania imeanza rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unaogharimu dola za Marekani bilioni 10, sawa na Shilingi trilioni 26. Mradi huo, unaotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), unatarajiwa kuwa bandari ya kibiashara kubwa zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji, bandari hiyo itajengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 800 na itakuwa na uwezo wa kuhudumia shehena ya kontena milioni 20 (TEUs) kwa mwaka. Hali hiyo itaifanya kuipiku Bandari ya Dar es Salaam kwa uwezo na ukubwa wa huduma zake.
Mbali na ujenzi wa bandari, mradi huo pia unahusisha kuanzishwa kwa Eneo Maalum la Uzalishaji (SEZ) lenye ukubwa wa hekta 1,700 litakalovutia viwanda na kuimarisha shughuli za biashara.
Bandari ya Bagamoyo inatarajiwa kuongeza ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafirishaji na biashara kimataifa, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.