GAIRO: DKT. SAMIA AHAHIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU NA HUDUMA ZA JAMII
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wananchi wa Gairo kwa hatua kubwa za kimaendeleo walizopiga katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, akisema wilaya hiyo imebadilika kwa kiwango kikubwa.
Akihutubia wananchi wa eneo hilo, Dkt. Samia ameahidi kuwa katika awamu ijayo serikali itaboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Rubeho–Kisitwi, Taboteli–Kitange, Chakwale–Mtumbatu na Chakwale–Leshata. Aidha, barabara ya Gairo–Nongwe itakamilishwa ili kurahisisha usafirishaji na kukuza shughuli za kiuchumi.
Katika sekta ya afya, amesema serikali itajenga vituo vitano vya afya katika kata za Lubeho, Idibo, Chakwale, Mandege na Leshata, pamoja na ujenzi wa zahanati 10 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kwa upande wa elimu na ajira, Dkt. Samia amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kukamilisha ujenzi wa chuo cha VETA Gairo ili vijana waweze kupata ujuzi, kujiajiri na pia kuajiriwa.
Akigusia sekta ya uchumi, ameahidi kujengwa kwa machinjio manne katika kata za Leshata, Twogwe, Kibedia na Italagwe. Vilevile, eneo la TANTRADE litakabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Gairo kwa ajili ya ujenzi wa soko kubwa katika kata ya Lubeho, huku pia ikipangwa kujengwa kwa stendi ya kisasa ya mabasi ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha huduma za usafiri.