KIBAIGWA - SAMIA ATAJA MAFANIKIO YA MAENDELEO KONGWA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, kufuatia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.
Akihutubia wananchi wa Kibaigwa, Dkt. Samia alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, nishati, barabara na kilimo.
Katika sekta ya elimu, shule za sekondari zimeongezeka na kufikia 45, huku sera ya elimu bila ada ikiendelea kutekelezwa. Aidha, serikali imekamilisha ujenzi wa chuo cha VETA kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3, kilichowawezesha vijana kujifunza fani mbalimbali kwa ajili ya ajira na kujiajiri.
Sekta ya afya nayo imepiga hatua, ambapo vituo vipya vya afya 14 vimejengwa na kufanya jumla kufikia 73. Pia, hospitali ya wilaya imepatiwa jengo jipya la huduma za dharura lenye thamani ya shilingi bilioni 4.5, lililowekwa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine mpya ya X-ray.
Kwa upande wa nishati, Rais Samia alisema vijiji vyote vya Kongwa sasa vina umeme, huku jitihada zikiendelea kufikisha huduma hiyo katika vitongoji na taasisi zote. Sub-station mpya pia imekamilika na kuanza kuhudumia wilaya za Gairo, Mpwapwa na Kongwa, hivyo kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme.
Katika sekta ya maji, visima 61 vimechimbwa na serikali imepanga kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika awamu ijayo.
Sekta ya miundombinu imeimarishwa kwa kuongezeka kwa barabara za lami kutoka kilomita 3.7 mwaka 2021 hadi 11.7 mwaka 2025. Pia, barabara ya Bonde la Mtanana yenye urefu wa kilomita 6 inatarajiwa kuboreshwa ili kudhibiti mafuriko.
Aidha, serikali imepanga kujenga vituo vya afya 10 na zahanati 21 pamoja na kukamilisha hospitali ya wilaya. Katika kilimo na mifugo, serikali itaendeleza minada 10 ya mifugo, majosho 35 na machinjio manne, sambamba na ujenzi wa eneo la maegesho ya malori kusaidia biashara kubwa za nafaka na bidhaa nyingine.
Rais Samia aliongeza kuwa kutokana na ongezeko la watu, shule mpya zitaendelea kujengwa Kibaigwa na maeneo mengine ya Kongwa, huku vyuo vya ufundi vikiboreshwa, na vitongoji vyote kuunganishwa na umeme.