Breaking News

KONGAMANO LA MAMA LISHE KAWE KUHAMASISHA MATUMIZI YA GESI SAFI KUFANYIKA AGOSTI 26 JIJINI DAR

Kikundi cha Mama Lishe Kawe “Ngome ya Mama” kwa kushirikiana na Kampuni ya Camgas - Camel Oil Ltd kimeandaa kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, litakalofanyika Agosti 26, 2025 katika Viwanja vya Msasani Beach, Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 21, 2025, Mratibu Mkuu wa Kongamano hilo, Potipoti Ndanga, amesema lengo ni kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya gesi safi ya kupikia ili kuachana na nishati chafu ikiwemo kuni na mkaa vinavyoathiri afya za watu na kuharibu mazingira.
Ndanga amesema maandalizi ya kongamano hilo yamehusisha utafiti kuanzia ngazi ya serikali za mitaa katika kata zote 20 za Manispaa ya Kinondoni, ambapo kila kata imetoa mwakilishi atakayeshiriki mashindano ya kumpata mpishi bora. Washiriki hao wanajumuisha wakina mama kutoka Kata 10 za Jimbo la Kawe na Kata 10 za Jimbo la Kinondoni.

“Lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa kusisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ikiwa Rais mwenyewe anatumia gesi safi majumbani, ni wajibu pia kwa wananchi kuacha kutumia nishati chafu na kuhamia kwenye gesi safi,” amesema Ndanga.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Kawe, Husna Nondo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, amesema matumizi ya nishati safi yatachochea mazingira safi na salama katika manispaa hiyo.

“Tunahamasisha kaya na wafanyabiashara wote kutumia nishati safi ya kupikia. Katika kongamano hili kutatolewa elimu ya matumizi bora ya gesi safi, kama ishara ya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Nondo.

Meneja Mkuu wa Camgas - Camel Oil Ltd, Sadiq Abrt, ambaye kampuni yake ni mdhamini mkuu wa kongamano hilo, amesema watatoa punguzo kwa wananchi watakaonunua majiko ya gesi siku ya tukio hilo ili kuongeza mwamko wa matumizi ya nishati safi.
Naye Balozi wa Camgas, Dotto Magari, amewataka wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kuhamia kwenye gesi safi ambayo haina madhara kwa afya wala mazingira.

Kwa upande wake, Zainabu Athuman Janguo, mlezi wa Kikundi cha Ngome ya Mama Samia (Wamachinga) Kawe, amesema kikundi hicho chenye wanachama 459 kitaendelea kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada za kusambaza nishati safi nchini.

“Kongamano hili tunalizindua rasmi hapa Kinondoni, lakini tunapanga kulipeleka pia katika mikoa mingine ya Dar es Salaam. Washindi wa mashindano ya upishi watapatiwa zawadi ikiwemo jiko la gesi,” amesema Janguo.